• HABARI MPYA

  Friday, July 27, 2012

  MTAKATIFU TOM AIONDOA YANGA MICHUANO MIPYA YA BENKI NA TFF

  Kocha Tom Saintfiet wa Yanga; MIchuano hii inakuja kuumiza wachezaji 
  Na Prince Akbar
  KOCHA wa Yanga, Tom Saintfiet raia wa Ubelgiji amesema michuano mipya ya ABC Bank Super 8 inakuja kuwaumiza wachezaji na binafsi yake, hayuko tayari kuingiza timu yake kwenye michuano hiyo.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY leo, Saintfiet alisema kwamba baada ya mashindano ya Klabu Bingwa ya soka Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame kesho ni vema wachezaji wakapewa muda wa kupumzika, badala ya kupewa adhabu nyingine.
  “Tunahitaji kupumzika, tunawaumiza wachezaji wetu, bado sijaambiwa rasmi, nimekamilisha programu yangu ya mazoezi leo (jana) na baada ya mechi na Azam, lazima wachezaji wangu wapumzike hadi Alhamisi. Ijumaa (Agosti 3) tunaanza upya programu ya mazoezi kwa ajili ya Ligi Kuu,”alisema Saintfiet.
  Michuano ya ABC Bank Super 8 inatarajiwa kuanza Agosti 4 hadi 18, ikishirikisha timu nane, nne za Zanzibar na nne za Bara.
  Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Angetile Osiah alisema jana kwamba timu tatu zilizoshika nafasi za juu katika Ligi Kuu zote mbili zitaingia moja kwa moja, wakati timu moja kila upande iiliyoongoza katika kampeni ya kupanda Ligi Kuu, zitashirikishwa pia.
  Alisema timu hizo zitakuwa katika makundi mawili na hakutakuwa na mechi ya kusaka mshindi wa tatu zaidi ya kuwepo kwa zawadi kwa timu itakayotwaa ubingwa tu na tayari wameshaziandikia barua za kuzitaarifu kuhusiana na michuano hiyo.
  “Nadhani hii ni nafasi nyingine kwa timu kuonyesha ushindani katika michuano hii, pia pamoja na kujiandaa kwa msimu mpya wa ligi, makocha wa timu shiriki wataweza kujua kiwango kilichopo kwenye timu zao na kama kuna kasoro warekebishe kabla ya kuanza kwa ligi,”alisema.
  Bank ABC ambayo imedhamini michuano hiyo kwa miaka mitatu, kupitia kwa Mkurugenzi wake Mkuu Boni Nyoni alisema wameamua kuandaa michuano hiyo ili kuunga mkono jitihada za maendeleo ya soka hapa nchini.
  Wakati kocha wa Yanga, washindi wa tatu wa Ligi Kuu ya Bara, Mtakatifu Tom akitoa msimamo huo, BIN ZUBEIRY inafahamu washindi wa pili wa ligi hiyo, Azam watakuwa na ziara ya wiki mbili nje ya nchi kujiandaa na msimu mpya.
  Aidha, mabingwa wa Ligi Kuu ya Bara, Simba SC, baada ya kutolewa wamewapa mapumziko wachezaji wake na watakutana wiki ijayo kuanza maandalizi ya tamasha lao la kilwa mwaka, Simba Day, litakalofanyika Agosti 8, mwaka huu na tayari wamekwishatoa ratiba yao kuanzia Agosti 5 hadi 11, mwaka huu.  
  Agosti 5, Simba itakuwa na Mkutano Mkuu wa mwaka katika ukumbi wa Polisi Oystrebay na siku hiyo hiyo watazindua Wiki ya Simba na Jamii, kuelekea Simba Day Agosti 6, watatembelea watoto yatima katika kituo cha Maungu Orphanage, Kinondoni Mkwajuni, Agosti 7, watatembelea wagonjwa katika hospitali ya Mwananyamala na Agosti 8, watafanya tamasha la Simba Day Uwanja wa Taifa, likitanguliwa na burudani kadhaa kabla ya mechi dhidi ya klabu moja kubwa barani.
  Agosti 9, Simba watatembelea shule ya msingi Mgulani kuhamasisha michezo mashuleni na Agosti 10, watatembelea kiwanda cha Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) Ilala, ambao ni wadhamini wao wakuu, kupitia bia ya Kilimanjaro Premium Lager.
  Tayari wadhamini wakuu wa Simba SC, kupitia Meneja wa bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe wamekwishakabidhi fedha, Sh. Milioni 20 kwa ajili ya Mkutano Mkuu na fedha nyingine za tamasha zitatolewa wiki ijayo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MTAKATIFU TOM AIONDOA YANGA MICHUANO MIPYA YA BENKI NA TFF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top