• HABARI MPYA

  Sunday, July 29, 2012

  HESHIMA IMERUDI DAR YOUNG AFRICANS AKA YANGA


  Yanga wakishangilia mwali wao wa Kagame

  Na Mahmoud Zubeiry
  MICHUANO ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame imefikia tamati jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa klabu ya Yanga, kufanikiwa kutetea taji lao, baada ya kuifunga Azam FC mabao 2-0.
  Shukrani kwao Hamisi Kiiza Diego na Said Bahanuzi, wafungaji wa mabao hayo moja kila kipindi na sasa Yanga inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, inaingia kwenye orodha ya mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo, kwa kutwaa taji hilo mara tano.
  Yanga sasa imebakiza mara moja kufikisha idadi sawa na wapinzani wao wa jadi, Simba (1974, 1991, 1992, 1995, 1996 na 2002) kutwaa Kombe hilo, mara tano kwa sita. Yanga ilibeba taji hilo 1975, 1993, 1999, 2011 na 2012.
  Kiiza alifunga bao lake, baada ya kuuwahi mpira aliokuwa anarudishiwa kipa Deo Munishi ‘Dida’ na beki Said Mourad na kumpiga chenga kipa huyo kisha kuusukuma mpira nyavuni.
  Bahanuzi aliuwahi mpira mrefu uliopigwa na beki Oscar Joshua na kuwazidi ujanja mabeki wa Azam kabla ya kumtungua Dida.
  Mechi hiyo ilichezeshwa vema na refa Thierry Nkurunzinza kutoka Burundi, aliyekuwa akisaidiwa na Simba Honore wa Rwanda na Peter Sabatia wa Kenya.
  Katika mchezo huo kikosi kilichoweka historia ya Kombe la tano la Kagame, Yanga SC kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Stefano Mwasyika, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Rashid Gumbo/Juma Seif ‘Kijiko’, Haruna Niyonzoma, Said Bahanuzi, Hamisi Kiiza na David Luhende.
  Azam FC; Deo Munishi ‘Dida’, Ibrahim Shikanda, Erasto Nyoni, Said Mourad, Aggrey Morris, Jabir Aziz, Kipre Tcheche/Mrisho Ngassa, Salum Abubakar, John Bocco ‘Adebayor’, Ibrahim Mwaipopo na Ramadhan Chombo ‘Redondo’. Benchi; Mwadini Ally, Samir Haji Nuhu, Joseph Owino, George Odhiambo, Mrisho Ngassa, Khamis Mcha ‘Vialli’ na Gaudence Mwaikimba.
  Katika mchezo uliotangulia wa kusaka mshindi wa tatu, AS ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) iliifunga APR ya Rwanda mabao 2-1, mabao yake yakifungwa na Magola Mapanda dakika ya 18 na Mutombo Kazadi dakika ya 67, wakati la kufutia machozi la timu ya jeshi la Rwanda, lilifungwa na Jean Mugiraneza dakika ya 89. 
  Ikumbukwe, Yanga ilikaribishwa kwenye michuano ya mwaka huu na kipigo cha 2-0 kutoka kwa Atletico ya Burundi katika Kundi C, kabla ya kushinda 7-1 dhidi ya Waw Salaam ya Sudan Kusini, na 2-0 dhidi ya APR ya Rwanda, ilishinda kwa penalti 5-3 dhidi ya Mafunzo katika Robo Fainali, kufuatia sare ya 1-1 na ikashinda 1-0 dhidi ya APR katika Nusu Fainali ndani ya dakika 120.
  Kikosi cha ubingwa jana;kutoka kulia ni Rashid Gumbo, Hamisi Kiiza, Nadir Cannavaro, Oscar Joshua, Kevin Yondan, Said Bahanuzi, Stefano Mwasyika, Haruna Niyonzima, David Luhende na Athumani Iddi. Mbele ni Ally Mustafa.
  Michuano hii, imemuibua kinara mpya wa mabao Yanga, Said Bahanuzi ‘Spider Man’, ambaye katika mabao 13 iliyofunga Yanga hadi sasa kwenye michuano ya mwaka huu, yeye amefunga sita, mengine matano Hamisi Kiiza ‘Diego’ na mengine mawili, moja Stefano Mwasyika na lingine Nizar Khalfan.
  Mafanikio haya yanajuka wiki mbili tu tangu Yanga ipate viongozi wapya, Mwenyekiti Yussuf Manji, Makamu wake Clement Sanga na Wajumbe Abdallah Bin Kleb, Mussa Katabaro, Aaron Nyanda na George Manyama.
  Yanga pia inajivunia udhamini wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia yake, Kilimanjaro Premeum Lager, ambao ni wa kwanza tangu wapoteze udhamini wa kampuni ya Shivacom.
  Ikumbukwe, Kilimanjaro Premium Lager ilianza kuidhamini Yanga Agosti 18, mwaka 2008, katika mkataba uliosainiwa kwenye hoteli ya Movenpick (sasa Serena), mjini Dar es Salaam.
  Kilimanjaro Premium Lager, ambao ni wadhamini wakuu wa wapinzani wa jadi wa Yanga, Simba SC, imekuwa ikihakikisha udhamini wake unafika maeneo yote muhimu katika shughuli za uendeshwaji wa klabu.
  Na inaaminika udhamini huo ndiyo chachu ya mafanikio ya miaka ya kmaribuni ya klabu hiyo, ikiwemo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu mara tatu katika kipindi cha miaka mitano (2008, 2009 na 2011) sambamba na ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame mwaka jana na mwaka huu.

  ILIVYOTWAA KOMBE MWAKA 2011:
  Yanga ilifanikiwa kutwaa taji la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame, 2011 baada ya kuifunga Simba bao 1-0, katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Shukrani kwake mshambuliaji wa kimataifa wa Ghana, Kenneth Asamoah aliyefunga bao hilo, pekee dakika ya 108, akiunganisha kwa kichwa krosi iliyochongwa kitaalamu na kiungo Rashid Gumbo.
  Kabla ya taji hilo walilotwaa Jumapili sambamba na dola za Kimarekani 30, 000, sawa na Sh. Milioni 45 za Tanzania, Yanga walitwaa tena Kombe hilo kwa mara ya kwanza mwaka 1975 kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar, wakiifunga Simba mabao 2-0 na baadaye mara mbili mjini Kampala, Uganda mwaka 1993 na 1999, mara zote wakiifunga SC Villa ya huko.
  Ulikuwa mchezo mgumu ambao ulidumu kwa dakika 120, timu zikionyesha kucheza tahadhari, kabla ya Asamoah kumaliza kazi.
  Kikosi kilichoipa Yanga kombe la nne la Kagame kilikuwa; Yaw Berko, Nsajigwa Shadrack, Oscar Joshua, Chacha Marwa, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Juma Seif ‘Kijiko’/Rashid Gumbo, Godfrey Taita/Julius Mrope, Nurdin Bakari, Davies Mwape, Jerry Tegete/Kenneth Asamoah na Hamisi Kiiza.
  Yanga iliyokuwa Kundi B la michuano ya mwaka huu, ilifuzu kama kinara wa kundi baada ya kujikusanyia pointi saba kutokana na kushinda mechi mbili na kutoka sare moja.
  Katika Robo Fainali, Yanga ilikutana na Red Sea ya Eritrea na kushinda kwa penalti 6-5, kufuatia sare ya bila kufungana ndani ya dakika 90 za mchezo huo.
  Katika Nusu Fainali, Yanga ilikutana na St George ya Ethiopia na kushinda tena kwa penalti 5-4, kufuatia sare ya bila kufungana ndani ya dakika 120, kabla ya kuiteketeza Simba SC katika fainali.
  Ikumbukwe katika michuano ya mwaka huu, Yanga iliingia kama ‘viti maalumu’, kwani Simba SC ndio walikuwa wawakilishi halisi kama mabingwa wa Bara.
  Ili kushiriki mashindano ya mwaka huu, ilibidi Yanga wailipe CECAFA dola za Kimarekani 20,000 kama faini ya kugomea mechi ya mshindi wa tatu wa michuano hiyo, mwaka 2008 mjini Dar es Salaam.
  Yanga ilitakiwa kucheza na Simba mwaka huo kuwania nafasi ya tatu, ikiwa chini ya Mwenyekiti aliyekuwa na misimamo mikali, Wakili Imani Omar Madega, Yanga iligoma kwa sababu hawakukubaliana na TFF juu ya mgawanyo wa mapato ya milangoni.  

  ZANZIBAR MWAKA 1975:
  Iliingia kama bingwa wa Tanzania baada ya kuifunga Simba SC katika fainali ya Ligi mwaka 1974 Uwanja wa Nyamagana, Mwanza, wakati watani wao hao waliingia kama mabingwa watetezi wa michuano.
  Yanga ilipangwa Kundi B pamoja na Express ya Uganda na Mufulira Wanderers ya Zambia. Yanga ilianza kwa kuifunga Express FC mabao 4-0 na baadaye kutoka sare ya 1-1 na Mufulira, hivyo kuongoza Kundi hilo na kukata tiketi ya kuingia Nusu Fainali.
  Katika Nusu Fainali, Yanga iliifunga Gor Mahia ya Kenya mabao 2-0 na kukata tiketi ya kuingia fainali Janauri 13, mwaka huo ilipokutana na watani wao wa jadi, Simba SC.
  Mabao ya Sunday Manara ‘Computer’ na Gibson Sembuli (sasa marehemu) yaliipa Yanga ushindi wa 2-0 na taji la kwanza la michuano hiyo.

  KAMPALA, UGANDA MWAKA 1993:
  Ilikwenda kama bingwa wa Bara na watano wao, Simba walikwenda kama watetezi wa taji na huko Yanga walipangwa Kundi A pamoja na wenyeji SC Villa na Malindi ya Zanzibar.
  Katika mchezo wa kwanza, Yanga ilifungwa 3-1 na Villa, siku hiyo kabla ya kuibuka na kuifunga Malindi mabao 2-1, yote yakitiwa kimiani na Said Nassor Mwamba ‘Kizota’, sasa marehemu, hivyo kukata tiketi ya kuingia Nusu Fainali.
  Katika Nusu Fainali, Yanga ilikutana na Express FC na kushinda mabao 3-1, hivyo kutinga fainali ambako ilikutana tena na SC Villa.
  Kwa kuzingatia matokeo ya mchezo wa awali kwenye Kundi A, Yanga haikupewa nafasi kabisa ya kufurukuta mbele ya SC Villa, lakini mambo yalikuwa tofauti, mabao ya Said Mwamba  na Edibily Lunyamila, yaliipa timu hiyo ushindi wa 2-1 pamoja na taji la pili la michuano hiyo.
  Marehemu Kizota aliibuka mfungaji bora wa michuano hiyo.

  KAMPALA, UGANDA MWAKA 1999:
  Ilikwenda kama bingwa wa Bara, ikiwa mwakilishi pekee na ilitua huko, huku mashabiki wengi wa soka Uganda wakiwa na kumbukumbu ya kile kilichofanywa na klabu hiyo mwaka 1993.
  Timu zilizoshiriki michuano hiyo ni Vital'O ya Burundi, Mebrat Hail ya Ethiopia, AFC Leopards ya Kenya, Kiyovu Sport, Rayon Sport za Rwanda,
  Naadiga Dekedaha ya Somalia, KMKM ya Zanzibar, Al Hilal ya Sudan, Yanga, wenyeji Express  na SC Villa za Uganda wakati Red Sea ya Eritrea ilijitoa dakika za mwishoni.
  Kwa matokeo hayo, Kundi D ilimokuwa Yanga lilibakiwa na timu mbili tu, yaani mabingwa hao wa Bara na mabingwa watetezi.
  Mechi ya kwanza, Yanga ilifungwa 3-0 na Rayon Januari 4 na ziliporudiana siku mbili baadaye, Yanga walilipa kisasi kwa ushindi wa 3-0 pia, mabao ya
  Sekilojo Chambua dakika ya 23 na 57 na Kali Ongala dakika ya 59.
  Katika Robo Fanali, Yanga ilikutana na Al Hilal Januari 10 na kushinda mabao 2-1, wafungaji Salvatory Edward dakika ya 14 na Edibily Lunyamila dakika ya 89 kwa penalti.
  Katika Nusu Fainali, Yanga ilikutana na Vital’O ya Burundi Januari 13 na kushinda mabao 3-2, wafungaji Kally Ongara dakika ya 16, Bakari Malima dakika ya 78 na Said Mhando dakika ya 90.
  Hivyo kwa mara ya pili, Yanga ilikutana na SC Villa kwenye fainali kukumbushia vitu vya mwaka 1993 na safari hii mambo yalikuwa mazito zaidi, kwani dakika 120 zilimalizika timu hizo zikiwa zimefungana bao 1-1 Lunyamila akiisawazishia Yanga dakika ya 42, baada ya Hassan Mubiru kutangulia kufunga dakika ya saba tu ya mchezo huo.
  Mchezo ukahamia kwenye mikwaju ya penalti na Manyika Peter akaingia kwenye orodha ya makipa hodari wa kupangua penalti baada ya kupangua mikwaju miwili, Yanga ikishinda kwa penalti 4-1, Uwanja wa Nakivubo.
  Hivyo ndivyo Yanga ilivyotwaa mataji yake matano ya Kombe la Kagame. Je, watawafikia wapinzani wa Simba mwakani? Bila shaka hilo ni jambo la kusubiri na kuona.
  Mwenyekiti wa Yanga, Yussuf Manji akisalimiana na Ngassa

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: HESHIMA IMERUDI DAR YOUNG AFRICANS AKA YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top