• HABARI MPYA

    Monday, July 23, 2012

    MILIONEA WA KIARABU AWAPA SIMBA UZI MKALI WA BEI MBAYA


    Wachezaji wa Simba muda si mrefu wataanza kung'aa na uzi mpya wa maana pigo za Man City

    Na Princess Asia
    KLABU ya soka ya Simba jana imepokea msaada wa jezi, raba, viatu vya kuchezea mpira, mabegi na suti za michezo (tracksuit) – vyote vya kisasa kabisa, kutoka kwa familia ya Al Ruwahi. Msaada huo umetolewa kwa mapenzi mema ambayo familia hiyo inayo kwa klabu.
    Ofisa Habari wa Simba SC, Ezekiel Kamwaga ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba mahusiano baina ya familia ya Al Ruwahi (Ruwehi) na Simba yamedumu kwa zaidi ya miaka 30 sasa. 
    Amesema takribani miaka 30 iliyopita, familia hiihii ilitoa zawadi ya basi (Nissan Coaster) kwa Simba na kuifanya klabu yetu kuwa ya kwanza nchini kumiliki basi lake yenyewe.
    Amesema msaada huo wa sasa kwa Simba una thamani ya Sh milioni 18 kwa ujumla wake na Simba sasa itavaa jezi hizo katika pambano lake la kesho dhidi ya Azam katika michuano ya Kombe la Kagame.
    Amesema klabu ya soka ya Simba inatumia nafasi hii kuwakaribisha wapenzi na wanachama wake kujitokeza kuisaidia klabu kwa namna yoyote ile, kama ilivyofanya familia hii ya Al Ruwahi, ili kusukuma mbele gurudumu la  maendeleo ya klabu.
    "Simba ni ya kila mmoja na haina mwenyewe. Umoja na mshikamano baina ya viongozi, wadhamini, wapenzi na wanachama wake, ndiyo utakaoifanya izidi kuwa bora hapa nchini na nje ya mipaka ya taifa letu,"alisema Kamwaga maarufu kama Mr. Liverpool.
    Wakati huo huo: Kamwaga amesema hali za wachezaji wa timu hiyo waliopo kambini katika hoteli ya Vina, Mabibo mjini Dar es Salaam zinaendelea vizuri tayari kwa mechi ya Robo Fainali, Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame kesho dhidi ya Azam. Amesema hadi sasa majeruhi ni mmoja tu, Amir Maftah na Abdallah Juma 'Dullah Mabao' amefanyiwa vipimo jana na majibu yake yanatolewa baadaye leo.
    Amesema kwa mujibu wa kanuni za mashindano haya, wachezaji wote waliokuwa na kadi moja ya njano kwenye hatua ya makundi wamefutiwa kadi zao na hivyo Simba itaingia uwanjani kesho Jumanne kwenye pambano dhidi ya Azam ikiwa haina mchezaji mwenye adhabu.
    Simba imesifiwa na CECAFA kuwa ni miongoni mwa timu zenye nidhamu nzuri kwenye michuano ya Kagame mwaka huu, mfano ukitolewa kwenye pambano lake dhidi ya AS VITA ya DR Congo, ambapo hakukuwapo na kadi yoyote iliyotolewa mechi nzima.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MILIONEA WA KIARABU AWAPA SIMBA UZI MKALI WA BEI MBAYA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top