• HABARI MPYA

  Saturday, July 28, 2012

  AZAM FC INAYOELEKEA ANGA ZA BEREKUM CHELSEA


  Kikosi chas Azam FC

  Prince Akbar
  KLABU ya Azam FC leo inacheza fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame dhidi ya mabingwa mara nne, Yanga SC, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Azam inakuwa klabu ya pili kihistoria, nje ya Simba na Yanga kucheza fainali ya michuano hiyo, baada ya Moro United mwaka 2006, ambayo ilifungwa 2-1 na Polisi Uganda, Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam mbele ya rais Jakaya Mrisho Kikwete, akiwa anakimbiza mwaka wake wa kwanza tangu aingie Ikulu.
  Hii timu ambayo inakimbiza miaka 10 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2004 na ipo kwenye mwaka wa tano tangu ianze kucheza Ligi Kuu mwaka 2008.
  Kocha Muingereza, Stewart Hall wa Azam FC iliyoitoa AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ili kuingia fainali, kwa kuifunga mabao 2-1, mabao yake yakifungwa na John Bocco ‘Adebayor’ na Mrisho Ngassa, anasema kwamba Yanga ni timu nzuri na fainali hiyo itakuwa ‘classic’, yaani baab kubwa.
  Katika miaka yake mitano ya kucheza Ligi Kuu, nuru ilianza kumulika kwenye anga zao mapema mwaka huu walipotwaa Kombe la Mapinduzi na baadaye Aprili, wakakata tiketi ya kucheza Kombe la Shirikisho la Soka Afrika, wakiwapiku vigogo, Yanga.
  Katika dunia ya leo, ambayo napokea mageuzi kisoka, hususan barani Afrika, timu kama Berekum Chelsea ya Ghana ikisumbua katika Ligi ya Mabingwa, kuna dalili za kutosha Azam inaelekea huko.
  Azam FC, kama ilivyokuwa kwa Mtibwa Sugar, nayo ilianzishwa na kikundi cha wafanyakazi wa kampuni ya Mzizima Flour Mill, kampuni tanzu ya Bakhresa, makao yake makuu yakiwa Barabara ya Nyerere, Dar es Salaam.
  Lengo la wafanyakazi hao wa kampuni inayomilikiwa na Said Salim Bakhresa, awali ilikuwa ni kucheza kwa ajili ya kujiburudisha, baada ya kazi.
  Lakini baada ya kuona wana timu nzuri, Oktoba 16, mwaka 2004, waliisajili rasmi kwa ajili ya kushiriki Ligi Daraja la Nne, wakitumia jina la Mzizima FC.
  Baadaye Mkurugenzi Mkuu wa makampuni ya Bakhresa, Abubakar Bakhresa, aliona ni vyema timu hiyo ihusishe wafanyakazi wa kampuni zote za Bakhresa, na kutumia jina la moja ya bidhaa zao kubwa, Azam.
  Kampuni nyingine za Bakhresa ni Food Products Ltd, Azam Bakeries Ltd, Omar Packaging Industries Ltd na kadhalika.
  Wazo lake lilikubaliwa na wafanyakazi wa kampuni hiyo, ndipo timu hiyo ikaanza kuitwa Azam SC, badala ya Mzizima. Lakini baadaye Juni 11, mwaka 2007, ilibadilishwa jina tena na kuwa Azam FC.
  Azam ilikwenda kwa kasi nzuri kuanzia Daraja la Nne na hadi mwaka 2008, ilifanikiwa kucheza Ligi Kuu, ikipandishwa na makocha King, aliyekuwa akisaidiwa na Habib Kondo. Baada ya kupanda, Azam ilimuajiri kocha wa zamani wa Simba SC, Mbrazil Neider dos Santos, aliyekuwa akisaidiwa na Sylvester Marsh na Juma Pondamali upande wa kuwanoa makipa.
  Baadaye ilimuongeza kocha wa viungo, Itamar Amorin kutoka Brazil pia, ambaye awali ya hapo alikuwa msaidizi wa Marcio Maximo katika timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
  Ilisajili pia wachezaji nyota, wazoefu, wakiwamo kutoka nje ya Tanzania, ambao walichanganywa na chipukizi wachache walioipandisha timu hiyo, kama John Bocco ‘Adebayor’.
  Wakati Azam inapigana kwenye Ligi Daraja la kwanza ili kupanda Ligi Kuu, kikosini ilikuwa ina wakongwe kama Shekhan Rashid na Suleiman Matola, viungo wa zamani wa klabu ya Simba.
  Malengo makuu ya Azam ni kuifanya timu iwe ya kulipwa, wachezaji wakihudumiwa vizuri, chini ya makocha bora, nao waweze kufanya vizuri na kuitangaza kimataifa timu hiyo na soka ya Tanzania kwa ujumla.
  Aidha, kwa kuwa inataka kutambulika kimataifa, ina kitengo maalumu cha soka ya vijana, kilicholenga kuibua vipaji vya chipukizi wa soka na kuwakuza katika misingi na maadili ya mchezo wenyewe, ili baadaye wauzwe Ulaya.
  Mmoja kati ya mabosi wa Azam, Yussuf Bakhresa, ni wakala wa wachezaji anayetambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), ambaye anaweza kuwafanya yosso wa klabu hiyo waende Ulaya moja kwa moja.
  Kikosi cha kwanza cha Azam Ligi Kuu kilikuwa kinaundwa na wafuatao; Kassim Kilungo, Said Bakar Nachikongo, Abdul Azizi Hamza, Shaaban Abdallah Kisiga ‘Malone’, Ally Suleiman Alawy, John Raphael Bocco ‘Adebayor’, Salum Machaku, Shekan Rashid Abdallah, Jamal Simba Mnyate, Yussuf Juma Gogo, Zuberi Ubwa, Yahaya Said Tumbo, Said Khamis Sued, Salum Abubakar Salum, Luckson Jonathan Kakolaki, Adam Shomari Ngido, Abdulhalim Chilumbe, Ngoy-Pichou Botwetwe, Mussa Khalid Kipao, Iddi Abubakar Mwinchumu, John Faustin Mabula, James Adriano Kilongola, Malika Philipo Ndeule, Paulo John Nyangwe, Abubakar Pawasa na Vladimir Niyonkuru.
  Azam pamoja na kumilikiwa na kampuni ya bilionea, zaidi ya basi lake ‘kali’, haina uwanja wake, Azam Complex, uliopo Chamazi, Mbagala, Dar es Salaam, ambao kwa msimu huu imeshuhudiwa hadi vigogo, Simba na Yanga wakiutumia kwa mechi zao za Ligi Kuu.
  Kwa sasa Kocha Mkuu wa Azam, Muingereza Stewart Hal. Naam, hao ndiyo Azam FC, wana Lamba Lamba.
  Hivi karibuni, Azam watafanya ziara ya kujiandaa na msimu mpya Falme za Kiarabu na inawezekana wakaondoka baada tu ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame inayofikia tamati leo mjini Dar es Salaam.
  Malengo ya Azam ni kutwaa Kombe la Kagame leo na kuhakikisha mwakani wanacheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho- pamoja na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Bara. Hao ndio Azam, wanaoelekea anga za Berekum Chelsea ya Ghana. 
  Mashabiki wa Azam FC

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AZAM FC INAYOELEKEA ANGA ZA BEREKUM CHELSEA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top