• HABARI MPYA

  Tuesday, July 24, 2012

  SPIDER MAN AFICHUA SIRI YA MAFANIKIO YAKE


  Spider Man; Said Bahanuzi akionyesha jezi namba yake

  Na Prince Akbar
  MSHAMBULIAJI mpya wa Yanga, Said Bahanuzi ‘Spider Man’ amesema kwamba siri ya mafanikio yake ni kujituma bila kukata tamaa uwanjani, bidii ya mazoezi na kusikiliza kwa makini na kufuata maelekeo ya kocha wake, Tom Saintfiet kutoka Ubelgiji.
  Bahanuzi aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na BIN ZUBEIRY jana, baada ya mechi ya Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame dhidi ya Mafunzo ya Zanzibar, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  “Nafurahi sana nimeanza vizuri katika timu yangu mpya, kwanza niseme namshukuru sana Mungu, lakini nawashukuru makocha wangu, kwa kuniamini na kunipa nafasi, hii inanijenga kujiamini na nahisi nilifanya uamuzi sahihi kusaini Yanga,”alisema.
  Lakini Bahanuzi amesema mafanikio haya ya mwanzoni hayatamfanya alewe sifa, badala yake ataendelea kujituma ili kujitengenezea mazingira ya kutimiza ndoto zake za kucheza Ulaya.
  Katika mchezo huo, ambao Yanga ilishinda kwa penalti 5-3 kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 90, Bahanuzi aliifungia bao la kusawazisha Yanga dakika ya 46, baada ya Ali Othman Mmanga, kutangulia kuifungia Mafunzo dakika ya 34, akiunganisha kona ya Juma Othman Mmanga.
  Kwa matokeo, hayo Yanga sasa itamenyana na APR ya Rwanda, kesho katika Nusu Fainali, mechi ambayo itakuwa ni ya pili kuzikutanisha timu hizo katika mashindano hayo, baada ya awali kukutana katika Kundi lao, C na Watoto wa Jangwani wakashinda 2-0, mabao yote akifunga Spider Man.
  APR yenyewe ilikata tiketi ya Nusu Fainali kwa kuitoa URA ya Uganda kwa kuifunga mabao 2-1, mabao yake yakifungwa na Jean Claude Iranzi dakika ya tisa na Suleiman Ndikumana dakika ya 34, wakati la Watoza Ushuru wa Kampala, lilifungwa na Robert Ssentongo dakika ya 57.
  Spider Man sasa anachuana vikali na mshambuliaji wa AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Taddy Atikiama katika mbio za kuwania kiatu cha dhahabu kwenye michuano hiyo, hadi sasa akiwa ana mabao matano sawa na mpinzani.
  Lakini bao moja Atikiama alifunga kwa penalti kwenye mechi ya mwisho ya Kundi A, dhidi ya mabingwa wa Tanzania, Simba SC.
  Ina maana, kama mwendo utakuwa huu hadi mwisho wa siku wachezaji hao kufungana kwa mabao, basi Bahanuzi atapewa kiatu cha dhahabu kwa sababu hana bao la penalti, zaidi ya alilofunga lao kwenye mechi dhidi ya Mafunzo katika penalti za kuamua mshindi baada ya sare ya 1-1 ndani ya dakika 90, ambalo halijaingizwa kwenye orodha ya mabao yake.
  Hamisi Kiiza ‘Diego’, nyota mwingine wa Yanga kutoka Uganda, anashika nafasi ya pili kwa mabao yake manne, akifuatiwa na Suleiman Ndikumana wa APR matatu, Abdallah Juma ‘Dullah Mabao’ wa Simba SC, Leonel St Preus wa APR, Didier Kavumbagu wa Atletico, Feni Ali na Robert Ssentongo wa URA, wote mabao mawili kila mmoja.

  WANAOONGOZA KWA MABAO:
  Taddy Etikiama                 AS Vita        5
  Said Bahanuzi                   Yanga SC     5
  Hamisi Kiiza                      Yanga SC     4
  Suleiman Ndikumana       APR             3
  Abdallah Juma                  Simba SC     2
  Leonel St Preus                 APR             2
  Didier Kavumbagu            Atletico         2
  Feni Ali                              URA             2
  Robert Ssentongo              URA             2


  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SPIDER MAN AFICHUA SIRI YA MAFANIKIO YAKE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top