• HABARI MPYA

  Saturday, January 09, 2016

  KOMBE LA MAPINDUZI 2016, NUSU FAINALI NI RAHA TUPU, KUJIAMINI KUMEWAPONZA AZAM

  Wachezaji wa Azam FC wenye mishahara mikubwa, Allan Wanga kutoka Kenya (kulia) na Kipre Tchetche wa Ivory Coast (kushoto) siku wanatolewa na Mafunzo kwa kufungwa 2-1 
  Na Mahmoud Zubeiry, ZANZIBAR
  KWA mara nyingine timu za Zanzibar zimeendelea kutolewa mapema katika michuano ya Kombe la Mapinduzi, mwaka huu zikiishia hatua ya makundi tu.
  JKU na Jamhuri zote zilizokuwa Kundi A na Mafunzo ya Kundi A zimerudishwa jukwaani kushuhudia michuano hiyo ikiendelea kuanzia hatua ya Nusu Fainali.
  Ajabu mwaka huu, mabingwa wa zamani wa Kombe la Mapinduzi, Azam FC wametolewa mapema katika mashindano hayo na hakuna kingine kilichowagharimu zaidi ya dharau na kujiamini.
  Azam FC waliingia katika mchezo wa kwanza mgumu dhidi ya Mtibwa Sugar na wakacheza kwa kiwango cha chini wakilazimisha sare ya 1-1.
  Lakini wakaenda kucheza kwa kujituma kwenye mchezo wa pili dhidi ya Yanga SC na kukaribia kushinda kama si beki Mtogo, Vincent Bossou kuwasawazishia wapinzani wao dakika za lala salama.
  Azam ikaamini itashinda mechi ya mwisho dhidi ya Mafunzo na kutinga Nusu Fainali, lakini matokeo yake ikafungwa 2-1 licha ya kuongoza 1-0 na hivyo kurudishwa Chamazi, Dar es Salaam.
  Ni aibu kwa wachezaji wa Azam kuonekana kwenye boti wanarejea Dar es Salaam wakati Kombe la Mapinduzi ndilo linaingia hatua ya Nusu Fainali.
  Kwa timu za Zanzibar, msimu huu zimeathiriwa na migogoro ya kisoka inayoendelea visiwani hapa, kiasi cha kusababisha washindwe kucheza hata Ligi.  Kumbuka mwaka jana, Polisi iliitoa KCC ya Uganda katika Nusu Fainali na JKU iliing’oa Yanga SC katika Robo Fainali, ingawa mwisho wa siku ni Simba SC waliotwaa ubingwa kwa kuwafunga Mtibwa Sugar kwa penalti.
  Kwa ujumla soka ya visiwani hapa imeathiriwa mno na mgogoro wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) dhidi ya wapinzani wao waliowafungulia kesi mahakamani.
  Yanga SC baada ya kutolewa mapema mwaka jana, mwaka huu ilionyesha dhamira ya tangu mapema kwamba imekuja kufanya kitu Zanzibar na haikuwa ajabu wameongoza Kundi B.
  URA ni timu ngumu na inacheza kwa nguvu na kasi kama Yanga SC, lakini bado mabingwa wa Bara wanapewa nafasi kubwa ya kwenda Fainali.
  Mtibwa Sugar ni timu ya ushindani siku zote katika mashindano haya, ikikumbukwa walilikosa kidogo taji hilo mwaka jana baada ya kufungwa kwa matuta na Simba SC.
  Na mwaka huu tena, Mtibwa Sugar wameendelea kuonyesha ni washindani wa taji – na watakutana na Simba SC katika marudino ya fainali ya mwaka jana.
  Simba SC na Mtibwa Sugar? Bonge la mechi hakuna shaka na patachimbika kweli Uwanja wa Amaan usiku wa kesho. 
  Mashabiki visiwani hapa watapenda sana Simba na Yanga ziingine Fainali, ili zikumbushie mechi ya mwisho ya mashindano hayo mwaka 2011 mabao ya Shijja Mkina na Mussa Mgosi yakiwapa ushindi wa 2-0 Wekundu wa Msimbazi.
  Mshambuliaji wa Simba SC, Danny Lyanga (kulia) akipambana na beki wa URA, Julius Ntambi (kushoto). URA itacheza na Yanga na Simba SC itacheza na Mtibwa Sugar katika Nusu Fainali kesho

  Ni kumbukumbu ambayo ipo kwamba mara ya mwisho wababe hao walipokutana kwenye michuano hiyo, Yanga SC ilitandikwa 2-0 na mahasimu, Simba SC.
  Nyavu zimetikiswa katika mashindano haya hadi sasa, lakini hajatokea mpachika mabao wa kutisha katika hatua yote ya makundi ya Kombe la Mapinduzi 2016.
  Aliyefunga mabao mengi ni mawili – na wapo watano ambao ni Awadh Juma wa Simba SC, Donald Ngoma wa Yanga SC, Villa Oramchani wa URA, Mohammed Abdallah wa JKU na Kipre Tchetche wa Azam FC.
  Wengine waliofanikiwa kuandika majina yao katika orodha ya wafungaji wa mabao kwenye Kombe la Mapinduzi mwaka huu ni Ibrahim Hajib,
  Jonas Mkude wote wa Simba SC, Vincent Bossou, 
  Paul Nonga na Malimi Busungu wote wa Yanga SC, 
  Oscar Agaba, Said Kyeyune wa URA, Emmanuel Martin, Nassor Juma wa JKU, Mwalim Mohammed na Ammy Mohammed wote wa Jamhuri.
  Beki wa Mtibwa Sugar, Salim Mbonde (kulia) akiondosha mpira mbele ya mshambuliaji wa Yanga SC, Donald Ngoma. Yanga itakutana na URA na Mtibwa na Simba kesho

  Wapo pia Shizza Kichuya, Hussein Javu na Said Bahanuzi wa Mtibwa Sugar, John Bocco wa Azam FC, Habib Sadik na Rashid Abdallah wa Mafunzo, ambao kila mmoja amefunga bao moja.
  Nusu Fainali zinatarajiwa kuchezwa kesho jioni na usiku na keshokutwa itakuwa mapumziko, wakati Jumanne Rais, Dk Ali Mohammed Shein anatarajiwa kukabidhi taji kwa bingwa wa mwaka huu wa Kombe la Mapinduzi.
  Nani atabeba mwali wa Mapinduzi 2016, Simba, Yanga, Mtibwa au URA? Bila shaka hilo ni jambo la kusubiri na kuona. Unaweza kuniita Bin Zubeiry. Asante kwa kusoma na endelea kutembelea BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE, tovuti nambari moja ya Kiswahili ya michezo duniani!
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KOMBE LA MAPINDUZI 2016, NUSU FAINALI NI RAHA TUPU, KUJIAMINI KUMEWAPONZA AZAM Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top