• HABARI MPYA

    Wednesday, January 20, 2016

    SIMBA SC YA MAYANJA HAPONI MTU, JKT AFA 2-0 TAIFA… SASA YANGA WAKAE CHONJO

    MATOKEO NA RATIBA LIGI KUU YA VODACOM TZ BARA…
    Januari 20, 2016
    JKT Ruvu 0-2 Simba SC
    Mgambo JKT 1-2 Azam FC
    Stand United 2-1 Toto Africans
    Ndanda FC 4-1 Mbeya City
    Prisons 2-1 Coastal Union
    Kesho; Januari 21, 2016
    Yanga SC Vs Majimaji
    Mwadui FC Vs Kagera Sugar
    African Sports Vs Mtibwa Sugar
    Hamisi Kiiza (kulia) akikimbia kushangilia huku akifuatwa na Emery Nimubona baada ya kufunga bao la kwanza

    Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
    SIMBA SC imeendeleza wimbi la ushindi chini ya kocha mpya, Mganda Jackson Mayanja baada ya jioni ya leo kuichapa JKT Ruvu mabao 2-0 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Ushindi huo unawafanya Wekundu wa Msimbazi wafikishe pointi 33 baada ya kucheza mechi 15, ingawa wanaendelea kukaa nafasi ya tatu nyuma ya Yanga SC yenye pointi 36 na Azam pointi 39. 
    Dakika 45 za kipindi cha kwanza zilimalizika bila mabao, huku JKT Ruvu wakicheza kwa nidhamu ya hali ya juu kujihami dhidi ya Simba SC.
    Beki Mrundi wa Simba SC, Emery Nimubona alikaribia kufunga dakika ya 25 kwa shuti akimalizia mpira uliotemwa na kipa Hamisi Seif kufuatia shuti la mshambuliaji Mganda, Hamisi Kiiza, lakini mpira ukaenda nje sentimita chache.
    Beki mwingine wa kushoto wa Simba SC, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ shuti lake kali lilidakwa na kipa wa JKT dakika ya 38.
    JKT nao hawakuwa wanyonge moja kwa moja, kwani dakika ya 38 Sesil Efrem alifumua shuti kali baada ya kupokea pasi kutoka kwa Samuel Kamuntu, lakini mpira ukaenda nje.
    Simba SC ilipata pigo dakika ya 43, baada ya beki tegemeo wa kushoto, Tshabalala kushindwa kuendelea na mchezo kufuatia kuchezewa rafu na Kamuntu – na nafasi yake kuchukuliwa na Abdi Banda.
    Kipindi cha pili, Simba SC walianza na mabadiliko, wakimpumzisha kiungo Peter Mwalyanzi na kumuingiza beki, Hassan Kessy ambaye kwa zaidi ya mwezi alikuwa nje kwa majeruhi.

    Mfungaji wa bao la pili la Simba SC, Danny Lyanga (kushoto) akimtoka beki wa JKT Ruvu leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
    Kikosi cha Simba SC kilichoichapa 2-0 JKT Ruvu leo Uwanja wa Taifa

    Mabadiliko hayo yaliisaidia Simba SC kupata bao lililofungwa na Kiiza kwa mkwaju wa penalti dakika ya 53, baada ya Sesil Efrem kumuangusha kwenye eneo la hatari Daniel Lyanga na refa Martin Saanya akatenga mpira kwenye boksi.
    JKT wakaonekana kuchanganyikiwa baada ya bao hilo na kuwpaa mwanya Simba SC kutekeleza mipango yao uwanjani na dakika ya 61 Lyanga akaifungia Simba bao la pili.
    Kipa Vincent Angban alipiga mpira mrefu ukatua katikati ya mabeki wawili wa JKT na Lyanga, aliyewazidi wote maarifa kabla ya kumlamba chenga na kipa wao kisha kusukumia ‘gozi’ nyavuni kuwaamsha vitini mashabiki wa Simba.
    Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Vincent Angban, Emery Nimubona, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’/Abdi Banda dk45, Hassan Isihaka, Juuko Murushid, Justice Majabvi, Mwinyi Kazimoto, Jonas Mkude, Hamisi Kiiza, Daniel Lyanga/Raphael Kiongera dk69 na Peter Mwalyanzi/Hassan Kessy dk46.
    JKT Ruvu; Hamisi Seif, Michael Aidan, Paul Mwidivi, Sesil Efrem, Nurdin Mohammed, Naftari Nashon, Hassan Dilungha, Issa Ngao/Amos Mgisa dk56, Samuel Kamuntu/Saad Kipanga dk81, Hamisi Thabit/Najim Magulu dk66 na Mussa Said.
    Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Stand United imeifunga Toto Africans ya Mwanza mabao 2-1 Uwanja wa kambarage mjini Shinyanga, Azam FC imeifunga Mgambo JKT 2-1 Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga, Ndanda FC imeifunga 4-1 Mbeya City Uwanja wa Nangwnada Sijaona, Mtwara na Prisons imeilaza 2-1 Coastal Union Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
    Ligi Kuu itaendelea kesho kwa mechi tatu, Yanga SC wakiikaribisha Majimaji Uwanja wa Taifa, Mwadui FC na Kagera Sugar Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga na African Sports na Mtibwa Sugar Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC YA MAYANJA HAPONI MTU, JKT AFA 2-0 TAIFA… SASA YANGA WAKAE CHONJO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top