• HABARI MPYA

    Monday, January 25, 2016

    JINI KISIRANI LAIKUMBA LIGI KUU, YANGA SC NAO WASEMA IJUMAA WANAKWENDA KAMBINI AFRIKA KUSINI

    Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
    KATIKA hali inayoashiria Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kukumbwa ‘Jini Kisirani’, Yanga SC imesema itaondoka nchini Ijumaa kwenda Afrika Kusini kuweka kambi ya kujiandaa na Ligi ya Mabingwa Afrika.
    Yanga SC inataka kuondoka nchini siku moja kabla ya mchezo wake wa Ligi Kuu dhidi ya Coastal Union ya Tanga uliopangwa kufanyika Jumamosi Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
    Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga SC, Jerry Muro ameiambia BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE leo kwamba kikosi cha timu yao kiinakwenda Afrika Kusini ili kuhakikisha wanapata maandalizi mazuri kabla ya kuanza kwa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwezi ujao.
    Yanga SC wanasema watakwenda Afrika Kusini Ijumaa

    Muro amesema Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Deusdedit Baraka atawasilisha barua ya kuomba kusogezwa kwa michezo yao kadhaa ili waweze kwenda Afrika Kusini.
    "Ni kweli Ijumaa tunakwenda Afrika Kusini kwa maandalizi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kama ambavyo inafahamika tutaanzia ugenini na Cercle de Joachim Februari 13, mwaka huu, ni hivi karibuni tu,”amesema Muro.
    Hatua ya Yanga inakuja baada ya mechi mbili za Ligi Kuu za Azam FC dhidi ya Prisons uliokuwa ufanyike Uwanja wa Sokoine, Mbeya Jumamosi wiki hii na dhidi ya Stand United uliopangwa kufanyika Februari 3, mwaka huu Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam kufutwa ili timu hiyo iende Azam FC Zambia.
    Azam FC inatarajiwa kuondoka usiku wa leo kwenda Zambia kushiriki michuano maalum na inatarajiwa kurejea Februari 4, mwaka huu.
    Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba ameiambia BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE leo kwamba wamepata ruhusa maalum kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) juu ya ziara yao na mechi zao hizo mbili za Ligi Kuu zitapangiwa tarehe nyingine.
    Kawemba amesema kwamba watakaporejea Februari 4, wataendelea na ratiba watakayoikuta ya Ligi Kuu, kuanzia mchezo na Mwadui FC Februari 7, Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
    Na Kawemba ameema mechi zao za viporo zitachomekwa katikati ya ratiba yao kuanzia hapo kulingana na nafasi ambayo itaonekana inafaa kwao na kwa wapinzani wao.
    Azam FC imealikwa nchini Zambia kushiriki michuano maalumu inayoshirikisha timu nne, iliyoandaliwa kwa ushirikiano wa klabu mbili za huko, Zesco United na Zanaco FC.
    Michuano hiyo itaanza keshokutwa Uwanja wa Levy Mwanawasa mjini Ndola na mbali na Azam FC, Zesco na Zanaco, timu nyingine itakayoshirki mabingwa wa Ligi Kuu Zimbabwe, Chicken Inn.
    Pamoja na Azam FC kuruhusiwa kwenda Zambia, Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea Jumamosi, Coastal Union wakiikaribisha Yanga SC Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na Simba SC wakiwa wenyeji wa African Sports wa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Mechi nyingine ni kati ya JKT Ruvu na Majimaji Uwanja wa Karume, Dar es Salaam, Mtibwa Sugar na Stand United Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro, Mwadui FC na Toto Africans Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga na Kagera Sugar dhidi ya Mbeya City Uwanja wa Mwinyi, Tabora. 
    Jumapili kutakuwa na mchezo mmoja tu, kati ya Mgambo JKT na Ndanda FC Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: JINI KISIRANI LAIKUMBA LIGI KUU, YANGA SC NAO WASEMA IJUMAA WANAKWENDA KAMBINI AFRIKA KUSINI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top