• HABARI MPYA

    Sunday, January 24, 2016

    AZAM FC WAPAA KESHO ZAMBIA KUSHIRIKI MICHUANO MAALUM

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC imealikwa nchini Zambia kushiriki michuano maalumu inayoshirikisha timu nne, iliyoandaliwa kwa ushirikiano wa klabu mbili za huko, Zesco United na Zanaco FC, itakayoanza kutimua vumbi Jumatano ijayo ndani ya Uwanja wa Levy Mwanawasa jijini Ndola nchini humo.
    Hii ni mara ya pili mfululizo kwa Azam FC kualikwa kwenye michuano hiyo iliyoanza mwaka 2014, mwaka jana ilishiriki kwa mara ya kwanza ilipofanyika jijini Lubumbashi, Congo DRC na TP Mazembe ikafanikiwa kuibuka mabingwa.
    Mwaka huu, Azam FC imealikwa kama mabingwa wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), huku pia ikishirikisha mabingwa wa Ligi Kuu Zimbabwe, Chicken Inn.
    Azam FC wanakwenda Zambia kesho kushiriki michuano maalum

    Timu nyingine zitakazoshiriki mwaka huu ni mabingwa wa Zambia, Zesco United na Zanaco ya huko, ambao walibeba ubingwa wa Ligi Kuu Zambia mwaka 2012.
    Malengo makubwa ya kuanzishwa michuano hiyo ni kuziandaa timu shiriki kuelekea msimu mpya wa ligi zao pamoja na michuano ya Afrika (CAF).
    Kwa mujibu wa historia ya michuano hiyo, timu ya Power Dynamos ya Zamzbia ndio timu ya kwanza kutwaa ubingwa huo mwaka juzi kabla ya mwaka jana kuchukuliwa na TP Mazembe, ambayo ilienda kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka jana.
    Timu shiriki za mwaka huu, Azam FC itaiwakilisha Tanzania mwaka huu kwenye Kombe la Shirikisho Afrika sawa na Zanaco itakayowakilisha kwa upande wa Zambia, huku Chicken Inn ikiiwakilisha Zimbabwe katika Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na Zecso United itakayopeperesha bendera ya Zambia katika michuano hiyo.
    Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, alisema kuwa kikosi hicho kitaondoka nchini kesho usiku kwa usafiri wa ndege mara baada ya kumaliza mchezo wa Kombe la Shirikisho (Azam Sports Confederation Cup) dhidi ya African Lyon.
    “Tutatumia michuano hiyo kama maandalizi yetu ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) na tunaamini itatusaidia vilivyo kukabiliana na mashindano yaliyopo mbele yetu,” alisema
    Kawemba aliwatoa hofu mashabiki wa timu hiyo ambao wamekuwa wakiifuatilia timu hiyo popote inapokuwa kwenye mechi zake nchini kwa kuwaambia kuwa watapata kushuhudia burudani ya mechi za Azam FC katika mechi zao huko kupitia televisheni ya Azam TV.
    Azam FC itaanza kuwania taji la michuano hiyo kwa kucheza na Zesco United Jumatano ijayo saa 10.00 jioni kwa saa za hapa, huku mchezo wa ufunguzi utakaoanza saa 8.00 mchana ukiwahusisha Zanaco watakaokipiga na Chicken Inn.
    Mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati watateremka tena dimbani saa 8.00 mchana Jumamosi ijayo kwa kukipiga na mabingwa wa Zimbabwe Chicken Inn, huku ukifuatiwa na ule baina ya wapinzani wa nchini humo Zesco na Zanaco utakaopigwa saa 10.00 jioni.
    Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB, itamalizia mechi yake ya mwisho Februari 3 mwaka huu kwa kukipiga na Zanaco, mchezo utakaoanza saa 10.00 jioni, utakaotanguliwa na ule baina ya Zesco na Chicken Inn utakaoanza saa 8.00 mchana.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM FC WAPAA KESHO ZAMBIA KUSHIRIKI MICHUANO MAALUM Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top