• HABARI MPYA

    Monday, January 25, 2016

    AYA 15 ZA SAID MDOE: BADO KUNA HAJA YA BENDI ZETU KUTOA ALBAM?

    KUNA wakati ilikuwa ni habari ya mjini pale linapokuja suala la bendi ya muziki wa dansi kuzindua albam mpya.
    Jiji la Dar es Salaam lilikuwa linazizima mwezi mzima kuelekea uzinduzi wa albam, bendi zikaweka kambi ili kujiandaa na tukio hilo muhimu.
    Kama vile hiyo haitoshi, mashabiki wa kutupwa kutoka miji mbali mbali ikiwemo Arusha, Moshi, Tanga na Morogoro, walikuwa wakihakikisha wanafunga safari kuja Dar es Salaam kushuhudia uzinduzi wa albam za bendi zao.
    Vituko vilivyokuwa vikiandamana kwenye uzinduzi wa albam navyo vilikuwa na ladha ya aina yake, mara Ally Chocky kaingia ukumbini na farasi, mara siku nyingine aingie na tinga tinga, mara aibukie juu ya paa la ukumbi wa Diamond Jubilee, mara Banza Stone aingie kama askari mwenye cheo cha juu (Jenerali).

    Muumin aingie na kundi la watu walioigiza kama waganga wa kienyeji, Badi Bakule aingie na jeneza, ili mradi kila staa wa bendi aliandaliwa kituko cha kuteka vichwa vya habari vya magazeti.
    Ukiachana na mbwembwe hizo, soko la albam ya muziki wa dansi lilikuwa juu sana miaka ya mwishoni mwa 90 hadi mieka ya 2000.
    Wasambazaji wakubwa wa kazi za muziki akina GMC na wengineo wakazithamini bendi zetu kiasi hata cha kuwapa mikopo ya kununua vyombo, kuweka kambi au ya kuingia studio kurekodi albam mpya. Hawakuwa na wasiwasi wa kutolipwa, muziki wa dansi ulikuwa unalipa.
    Lakini taratibu mambo yakaanza kubadilika, albam zikaanza kupunguza umaarufu sokoni, wasambazaji wakaanza kuangalia upepo mwingine, wakachungulia kwenye taarab na muziki wa injili.
    Sasa hivi ukizindua albam basi uwezekano wa kupata hasara ni mkubwa sana, kwa kifupi albam za muziki wa dansi hazilipi tena.
    Na ndipo hapo ninaposhawishika kuuliza, je bado kuna haja ya bendi zetu kutoa albam? Na kama upo ulazima, je kuna haja ya kuzifanyia show kubwa za uzinduzi?
    Katika miaka ya hivi karibuni, mara kadhaa tumeshuhudia bendi zikizindua albam mpya lakini ukumbini hakuna hata CD moja ya albam mpya, mfano wa karibu ni pale FM Academia ilipozindua albam ya “Chuki ya Nini” pale Mzalendo Pub - Millennium Tower huku wakiwa hawana nakala hata moja mkononi.
    Hiyo inaonyesha namna ambavyo suala la kuzindua albam lilivyopoteza heshima hata kwa bendi zetu zenyewe na matokeo yake matukio ya uzinduzi kupelekwa bora liende.
    Kama tunasema nyimbo za dansi hazipigwi radioni, kama albam haziuziki, kama wasambazaji hawautaki muziki wa dansi, kama bendi zinaweza kugawa nyimbo mpya bure hadi kwa whatsapp, kuna haja gani ya kutoa albam?
    Soko la muziki limebadilika na sasa njia kuu iliyobakia ya bendi kupata kipato, ni maonyesho ya kila siku kwenye kumbi za starehe, hakuna njia nyingine na wala watu wa masoko wa bendi zetu (kama wapo) hawana maarifa ya kutafuta njia nyingine ya kuziingizia kipato bendi.
    Kama tumekubali kuwa kipato ni cha mlangoni tu basi angalau kwa kipindi hiki (ambacho labda ni cha mpito) bendi zingejikita kutoa wimbo mmoja (audio na video) kila baada ya kipindi fulani na kuufanyia juhudi za makusudi ili uchezwe kwenye vituo vya radio na televisheni, kwenye mitandao na kwingineko na isitoe ngoma nyingine kabla haijajiridhisha kuwa wimbo uliotangulia umechuja sokoni.
    Hii maanake nini? Maanake ni kwamba wimbo uking’ara basi ni wazi kuwa mashabiki nao wataongezeka kwenye kumbi za dansi, ni rahisi kuweka nguvu kwenye wimbo mmoja badala ya albam nzima na ni ukweli usio na ubishi kuwa kuachia nyimbo mbili au zaidi kwa wakati mmoja kunachangia wimbo mmoja au zote kupotea kirahisi
    Kama kuna haja ya kutoa albam kwa soko lala sasa basi iwe tu ni kwaajili ya kulinda kumbukumbu na historia ya bendi na hili linaweza kufanywa kwa kukusanya zile nyimbo moja moja (single) zilizokuwa zikiachiwa kila baada ya kipindi Fulani. Tusome alama za nyakati, tusilazimishe vitu ambavyo havina tija.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AYA 15 ZA SAID MDOE: BADO KUNA HAJA YA BENDI ZETU KUTOA ALBAM? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top