• HABARI MPYA

    Wednesday, January 27, 2016

    SAMATTA ANAONDOKA USIKU HUU DAR KWENDA UBELGIJI KUKAMILISHA USAJILI WAKE KRC GENK

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    NAHODHA wa Tanzania, Mbwan Ally Samatta yuko Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam anasubiri kupanda ndege ya KLM kwenda Ubelgiji.
    Samatta anaondoka Saa 6:00 usiku wa leo kwenda Ubelgiji kukamilisha taratibu za kujiunga na KRC Genk ya Ligi Kuu ya Ubelgiji, baada ya klabu yake, TP Mazembe kukubali kumuuza.
    Bilionea Moise Katumbi Chapwe, Rais wa klabu ya TP Mazembe ya DRC amekubali mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Tanzania akajiunge na KRC Genk, badala ya Nantes na Marseille za Ufaransa zilizokuwa zinamtaka pia.
    BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE inafahamu Samatta tayari amekwishasaini Mkataba wa awali na Genk wa miaka minne na sasa anakwenda kukamilisha taratibu.
    Mbwana Samatta (kulia) yuko JNIA anasubiri kupanda ndege ya KLM kwenda Ubelgiji

    Samatta na Genk wanataka kukimbizana na muda ili kuwahi kabla ya dirisha dogo la usajili  halijafungwa, angalau mapema Februari Mwanasoka huyo Bora Anayecheza Afrika aanze kucheza Ubelgiji.
    Samatta aliondoka Dar es Salaam Januari 20, akiwa ameambatana na Ofisa mmoja wa Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo kwenda Lubumbashi, DRC kumshawishi Katumbi akubali ofa ya Genk.
    Katumbi alikuwa anataka Samatta aende Nantes ya Ufaransa, ambao walikuwa tayari kuilipa Mazembe Euro Milioni 1 na kuipa asilimia 25 ya mgawo iwapo watamuuza klabu nyingine mchezaji huyo. 
    BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE inafahamu Genk wamekubali kutoa Euro 800,000 kumnunua Samatta kutoka Mazembe na kutoa asilimia 20 ya ngawo kwa klabu ya Lubumbashi iwapo itamuuza Samatta klabu nyingine.
    Samatta aliyejiunga na TPM mwaka 2011 akitokea Simba SC aliyoichezea kwa nusu msimu, akitokea African Lyon, hadi sasa ameichezea klabu hiyo mechi 103 na kuifungia mabao 60.
    Ndani ya mechi hizo, kijana huyo wa umri wa miaka 24, ameshinda taji la Ligi ya Mabingwa Afrika na Mazembe, huku naye akiibuka mfungaji bora wa michuano hiyo na kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora Anayecheza Afrika.   
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SAMATTA ANAONDOKA USIKU HUU DAR KWENDA UBELGIJI KUKAMILISHA USAJILI WAKE KRC GENK Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top