• HABARI MPYA

  Wednesday, August 10, 2016

  SIMBA WAMEFANIKIWA KUUNDA TIMU NZURI, SASA WAJIFUNZE KUSTAHMILI

  KAMA walivyosema wahenga kwamba nyota njema huonekana asubuhi, basi Simba SC wamekuwa na mwanzo mzuri msimu huu.
  Hiyo inafuatia kusherehekea vizuri miaka 80 ya klabu yao juzi baada ya kuifunga AFC Leopard ya Kenya mabao 4-0 katika mchezo wa kirafiki Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Mshambuliaji chipukizi wa kimataifa wa Tanzania, Ibrahim Hajib Migomba, au Cadabra wakimfananisha na mshambuliaji mpya wa Manchester United, Zlatan Ibrahimovic aliendelea kumvutia kocha mpya, Mcameroon Joseph Marius Omog baada ya kufunga mabao mawili, huku wachezaji wapya, Mrundi Laudit Mavugo na Shizza Kichuya wakifunga pia. 
  Simba walikwenda kupumzika wakiwa wanaongoza kwa bao 1-0 lililofungwa na Hajib dakika ya 38 kwa shuti la umbali wa mita takriban 30 baada ya kupokea pasi ya kiungo Mkongo, Mussa Ndusha.
  Kwa bao lile, acha niseme Hajib ameingia katika orodha ya wachezaji ninaowapenda kibinafsi, ambao nawashangilia bila kujali wanacheza timu gani.
  Hajib alipewa pasi akiwa umbali wa mita 30 na wengi tukajua alipewa pasi katika mipango ya Simba kuzidi kuusogeza mpira kwenye eneo la wapinzani.
  Lakini yeye baada ya kupokea pasi, akainua sura kuangalia mbele, akagundua kipa amekaa mkao wa kufungwa na kuna njia ya kuupitisha mpira hadi nyavuni, basi akafumua shuti na kufunga.
  Bao la Hajib lilikuja wakati AFC Leopard ndiyo wanatawala mchezo na mashabiki wa Simba walikuwa kimya, walioonekana kujikatia tamaa.
  Bao hilo likaamsha ari ya Simba SC kwa ujumla kuanzia mashabiki, benchi la Ufundi na wachezaji wenyewe na kipindi cha pili Hajib akamalizia vizuri krosi ya Kichuya kuifungia Simba SC bao la pili dakika ya 56.
  Kichuya naye akawainua vitini mashabiki wa Simba SC walioongozwa na Rais wa klabu, Evans Elieza Aveva na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwa kufunga bao la tatu dakika ya 66, akimalizia krosi ya Mavugo.
  Mavugo aliyejiunga na Simba SC mwishoni mwa wiki, akaifungia timu hiyo bao la nne dakika ya 82 
  akiunganisha krosi nzuri ya Kichuya, aliyekuwa nyota wa mchezo wa huo.
  Ushindi huo uliletwa na; Vincent Angban, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Janvier Besala Bokungu aliyempisha Hamad Juma dakika ya 72, Novaty Lufunga, Method Mwanjali aliyempisha Juuko Murshid dakika ya 77, Jonas Mkude, Mwinyi Kazimoto aliyempisha Jamal Mnyate dakika ya 46, Mussa Ndusha aliyempisha Muzamil Yassin dakika ya 46, Frederick Blagnon aliyempisha Laudit Mavugo dakika ya 46, Ibrahim Hajib alioyempisha Mohamed Ibrahim dakika ya 67 na Shizza Kichuya ambaye unaweza kusema alikuwa nyota mchezo.
  Kwa kutazama wachezaji waliotumika katika mchezo huo, waliobaki benchi na ambao walikuwa jukwaani, inatosha kusema Simba SC wamefanikiwa kuunda timu nzuri msimu huu.
  Katika waliokuwa benchi ni Dennis Richard pekee ambaye hakuingia na wengine walikuwa jukwaani kabisa kama Malika Ndeule, Said Ndemla, Danny Lyanga, Ame Ali na Peter Manyika.
  Simba SC wanafanikiwa kuunda timu nzuri yenye uwiano mzuri wa wachezaji kwa nafasi na umri baada ya misimu kadhaa ya kuendesha zoezi hilo ovyo.
  Na baada ya kufanikiwa katika dhana ya kuunda timu, mtihani uliopo mbele ya viongozi wa Simba sasa ni kuweza kutekeleza yaliyomo kwenye mikataba ya wachezaji, kuistahmilia timu izoeane na hatimaye kuanza kufanya vizuri na kuleta mataji.
  Haimaanishi baada ya usajili huo eti Simba watakuwa wanashinda kila mechi, ama watatwaa taji msimu huu lazima, au ndiyo wataifunga Yanga – hapana, mambo mazuri hayataki haraka na umefika wakati sasa Simba wajfunze ustahmilifu. Alamsiki.    
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA WAMEFANIKIWA KUUNDA TIMU NZURI, SASA WAJIFUNZE KUSTAHMILI Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top