• HABARI MPYA

    Sunday, August 21, 2016

    SERENGETI BOYS YAIPIGA AFRIKA KUSINI 2-0 NA KUSONGA MBELE MICHUANO YA AFRIKA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    TIMU ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Tanzania imefuzu hatua ya mwisho ya mchujo wa kuwania tiketi ya Fainali za Afrika mwakani Madagascar, baada ya kuifunga Afrika Kusini mabao 2-0 jioni ya leo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
    Serengeti Boys inafuzu kwa ushindi wa jumla wa 3-1 baada ya sare ya 1-1 katika mchezo wa kwanza Afrika Kusini na katika hatua ya mwisho ya mchujo wa kuwania tiketi ya Madagascar mwakani, sasa itamenyana na Kongo Brazaville iliyoitoa Namibia.
    Ahsante nyingi kwao, wafungaji wa mabao hayo leo, Mohamed Rashid Abdallah kipindi cha kwanza na Muhsin Malima Makame kipindi cha pili.
    Pamoja na ushindi huo, Tanzania maarufu kama Serengeti Boys ililazimika kucheza pungufu tangu dakika ya 44 baada ya kiungo wake wa ulinzi, Ally Hamisi Ng’anzi kuonyeshwa kadi ya pili ya njano na kutolewa kwa kadi nyekundu.
    Wachezaji wa Serengeti Boys wakifurahia ushindi wao leo Chamazi
    Serengeti Boys ilipata bao lake la kwanza dakika ya 34 baada ya Mohamed Rashid Abdallah kumalizia vizuri pasi ya Yohana Nkomola kumtungua kipa wa Amajimbos Glen Tumelo Baadjes.
    Benchi la Ufundi la Serengeti Boys, chini ya Mkurugenzi wa Ufundi, Mdenmark Kim Poulsen, Kocha Mkuu, Bakari Shime na Kocha wa makipa, Muharami Mohammed ‘Shilton’, lilirudi na mipango mizuri kipindi cha pili na timu ikaendelea kutawala mchezo licha ya kucheza pungufu.     
    Haikuwa ajabu Muhsin Malima Makame alipoifungia bao Serengeti bao la pili dakika ya 83 kwa shuti akimalizia krosi ya Mohamed Rashid Abdallah.
    Mfungaji wa bao la kwanza la Serengeti Boys, Mohamed Abdallah akimtoka beki wa Amajimbos, Kwenzokuhle Shinga 
    Kiungo wa Serengeti akimtoka Luke Donn wa Amajimbos  
    Kevin Naftal wa Serengeti Boys akimtoka mchezaji wa Amajimbos Luke Gareth
    Mashabiki wakifurahia burudani ya Serengeti Boys leo Chamazi

    Bao hilo liliwavunja nguvu kabisa Amajimbos walio chini ya kocha Moleti Ntseki anayesaidiwa na Shawn Bishop na kuanza kucheza ili kutoruhusu mabao zaidi. 
    Ushindi huu ni sawa kisasi kwa Afrika Kusini ambayo mwaka jana iliitoa Serengeti Boys katika hatua hii kwa jumla ya mabao 5-1, wakishinda 4-0 kwao na kutoa sare ya 1-1 Dar es Salaam.
    Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Ramadhan Kambwili, Ally Msengi, Nickson Kibabage, Israel Mwenda, Ally Ng’anzi, Kelvin Naftal, Shaaban Zubeiry, Mohamed Abdallah, Yohana Nkomola na Asad Ali. 
    Afrioka Kusini; Glen Tumelo, Luke Gareth, Luke Donn, Mswati Lukhele, James Thabiso, Jaqueel De Jagher, Kwenzokuhle Shinga, Siphamandla Ntuli, Mjabulise Mkhize, Linamandla Mchilizeli na Mdamolelo Radzilane. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SERENGETI BOYS YAIPIGA AFRIKA KUSINI 2-0 NA KUSONGA MBELE MICHUANO YA AFRIKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top