• HABARI MPYA

    Sunday, August 21, 2016

    YANGA VETERANI MABINGWA KOMBE LA AZAM FRESCO

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    TIMU ya Yanga Veterani usiku wa leo imefanikiwa kutwaa ubingwa wa michuano ya Kombe la Azam Fresco baada ya kuifunga Mbagala Kuu mabao 2-1 Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
    Kwa kutwaa ubingwa wa michuano hiyo, Yanga imezawadiwa fedha taslimu Sh. Milioni 1, wakati Mbagala Kuu imepewa Sh. 500,000 kwa kushika nafasi ya pili.
    Refa Baraka Rashid alikataa bao zuri la kiungo Ally Yussuf ‘Tigana’ dakika ya 20 baada ya kupiga shuti la umbali wa mita 20 lililogonga mwamba wa juu ndani na kudondea mstari wa ndani wa lango, lakini mwamuzi ‘akaminya’.
    Mwakilishi wa kampuni ya Bakhresa Group, Jaffar Iddi (kushoto) akimkabidhi Nahodha wa Yanga, Ally Yussuf 'Tigana' Kombe la Azam Fresco 2016  
    Mshambuliaji wa Yanga, Kipanya Malapa akimtoka beki wa Mbagala Kuu leo Chamazi
    Wachezaji wa Yanga wakifurahia na Kombe lao leo Uwanja wa Azam Complex

    Hata hivyo, Tigana akawainua tena vitini mashabiki wa Yanga dakika ya 27 baada ya kumalizia pasi ya Gulla Joshua kufuatia kazi nzuri ya beki wa kulia Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’ aliyepandisha shambulizi.
    Rajab Risasi akaisawazishia kwa penalti Mbagala Kuu dakika ya 50 baada ya Willy Mtendamema kuunawa mpira kwenye boksi.
    Paschal Kaliasa aliyecheza nafasi ya kiungo wa ulinzi leo, akaifungia bao la ushindi Yanga Veterani dakika ya 65 kwa shuti la mpira wa adhabu, baada ya Athumani China kuangushwa nje kidogo ya boksi.
    Aziz Hunter akaifungia Yanga bao ambalo lingekuwa la tatu akimalizia krosi ya Bakari Malima, lakini refa akasema alikuwa ameotea kabla ya kutumbuza mpira nyavuni.
    Baada ya mchezo huo, Mwakilishi wa kampuni ya Bakhresa iliyoandaa mashindano hayo, Jaffar Iddi Maganga akakabidhi zawadi za fedha, jezi na vikombe kwa washindi wote.
    Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Athumani Abdallah, Nsajigwa Shadrack, Bakari Malima, Willy Mtendamema, Hamad Said, Paschal Kalyasa, Abdallah Suleiman ‘Kaburu’/Athumani China dk36, Ally Yussuf ‘Tigana’, Gulla Joshua, Kipanya Malapa/Aziz Hunter dk38 na Deo Lucas/Saaleh Hilal dk68.
    Mbagala Kuu; Idd Kalenga, Adam Matola/Ramadhani Madebe 38, Seleta Felix, Rama Suzuki, Dullah Mukulu, Kondo S Kondo, Teacher Selemani/Alifu dk40, Rajab Risasi, Heri Morris, Abdulrahman Ssentongo na Edgar. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA VETERANI MABINGWA KOMBE LA AZAM FRESCO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top