• HABARI MPYA

    Tuesday, August 30, 2016

    YANGA WAKACHA KESI YA KESSY TFF, WAAMBIWA WASIPOTOKEA NA JUMAPILI IMEKULA KWAO

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KAMATI ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji Jumapili ya Septemba 4, 2016 inatarajiwa kutoa hukumu ya shauri la mchezaji Hassan Ramadhan Kessy anayedaiwa na Klabu ya Simba kuvunja mkataba kwa kuanza kufanya mazoezi na klabu ya Young Africans sambamba na kusajili katika timu hiyo ya Mtaa wa Jangwani, Dar es Salaam kabla ya mkataba wake kufika mwisho Juni 15, 2016.
    Simba imelalamika mbele ya kamati hiyo ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuwa, mchezaji Hassan Kessy alivunja taratibu hizo akiwa ndani ya mkataba wa klabu hiyo yenye mashakani yake Barabara ya Msimbazi jijini Dar es Salaam.
    Hassan Kessy (kushoto) akiichezea Yanga dhidi ya African Lyon Jumapili
    Kwa mujibu wa taarifa ya Kamati hiyo, shauri hilo lilisikilizwa na uamuzi wake utatolewa Jumapili ijayo. Hii ni baada ya kushindikana kusikilizwa kwa shauri jingine linalohusu Klabu Simba ikiilalamikia Klabu Young Africans, kuingia mkataba na mchezaji Hassan Ramadhani Kessy wakati bado ana mkataba na klabu Simba.
    Shauri la Simba dhidi ya Young Africans lilishindika kusikilizwa kwa sababu Young Africans hawakutokea mbele ya kamati hiyo wakati wa kusikiliza shauri hilo, hivyo kamati itaiandikia barua Young Africans kukumbushwa kuhudhuria kwenye kesi hiyo Jumapili ijayo kabla ya kutolewa uamuzi. Kama hawakutokea tena, shauri hilo litasikilizwa upande mmoja na kutolewa uamuzi upande mmoja.
    Katika hatua nyingine, Chama cha Wachezaji wa Mpira wa Miguu Tanzania (SPUTANZA), kilileta malalamiko dhidi ya Yanga kuhusu madai ya usajili wa Jerry Tegete, Omega Seme na Hamisi Thabiti. 
    Shauri hilo sasa litasikilizwa Jumapili ijayo ya Septemba 4, 2016 baada ya kushindikana kusikilizwa kutokana na mdaiwa Yanga kutotokea kwenye kesi. Yanga imeagizwa kukuhudhuria shauri hilo vinginevyo litasikilizwa upande mmoja na kutolewa uamuzi upande mmoja.
    Nayo Coastal Union ilileta malalamiko dhidi ya Yanga kuhusu madai ya fidia ya mchezaji Juma Mahadhi. Shauri hili sasa litasikilizwa Jumapili ijayo ya Septemba 4, 2016 baada ya kushindikana kusikilizwa kutokana na mdaiwa Yanga Africans kutotokea kwenye kesi. Yanga wameagizwa kukuhudhuria shauri hilo, vinginevyo litasikilizwa upande mmoja na kutolewa uamuzi upande mmoja.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA WAKACHA KESI YA KESSY TFF, WAAMBIWA WASIPOTOKEA NA JUMAPILI IMEKULA KWAO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top