• HABARI MPYA

    Sunday, August 28, 2016

    YANGA YAANZA NA MOTO LIGI KUU, YAITANDIKA 3-0 AFRICAN LYON

    Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
    MABINGWA watetezi, Yanga SC wameanza vizuri Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya kushinda mabao 3-0 dhidi ya African Lyon Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Pongezi kwa wafungaji wa mabao hayo, viungo Deus David Kaseke aliyefungua biashara nzuri kipindi cha kwanza, Simon Msuva na Juma Mahadhi.
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Rajab Mrope wa Ruvuma, Mirambo Tshikungu wa Mbeya na Janeth Balama wa Iringa, hadi mapumziko Yanga walikuwa mbele kwa bao 1-0.
    Bao hilo lilifungwa na Kaseke dakika ya 18, akimalizia pasi ya winga Simon Msuva, ambaye leo alikuwa katika kiwango chake.
    Mfungaji wa bao la kwanza la Yanga, Deus Kaseke akifurahia kwa ishara kwenye kibendera leo. Kushoto ni Donald Ngoma

    Baada ya bao hilo, Yanga iliongeza kasi ya mashambulizi, lakini Lyon iliyokuwa ikiwategeshea mitego ya kuotea wapinzani wao, haikuweza kuruhusu bao lingine. 
    Kipindi cha pili, Yanga SC inayofundishwa na kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm ilirejea vizuri zaidi na kufanikiwa kutawala zaidi mchezo.
    Haikuwa ajabu mabingwa hao watetezi walipopata mabao mawili zaidi kipindi hicho na kuamsha shangwe zaidi za mashabiki wake.
    Simon Msuva alifunga bao la pili dakika ya 60 akimlamba chenga kipa Mcameroon Youthe Rostand baada ya pasi ya Mzimbabwe Thabani Kamusoko kabla ya Juma Mahadhi kufunga la tatu dakika ya 90, akimalizia pasi ya kinda Yussuf Mhilu.
    Mshambuliaji wa Yanga, Donald Ngoma akimtoka beki wa African Lyon, Hamad Tajiri
     Kiungo Deus Kaseke akimtoka beki wa Lyon, William Otong  
    Mshambuliaji wa Yanga SC, Amissi Tambwe akifumua shuti katikati ya wachezaji wa African Lyon 
    Beki wa Yanga, Hassan Kessy (kushoto) akipoga krosi pembeni ya wachezaji wa Lyon
    Winga wa Yanga, Simon Msuva akimtok beki wa Lyon, Amani Peter

    Mchezo mwingine wa Ligi Kuu leo, bao pekee la beki Haruna Shamte limeipa Mbeya City ushindi wa 1-0 dhidi ya timu yake ya zamani, Toto African Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
    Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Hassan Kessy, Mwinyi Hajji, Andrew Vincent, Vincent Bossou, Simon Msuva/Juma Mahadhi dk76, Thabani Kamusoko, Donald Ngoma/Matheo SImon dk88, Amissi Tambwe na Deus Kaseke/Yussuf Mhilu dk89. 
    African Lyon; Youthe Rostand, Baraka Jaffar, Halfan Twenye, Hamad Tajiri, William Otong, Omar Salum, Amani Peter/Awadh Juma dk46, Mussa Nampaka/Abdul Hilal dk74, Omary Abdallah/Ramadhani Kipalamoto dk74, Hood Mayanja na Tito Okello.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA YAANZA NA MOTO LIGI KUU, YAITANDIKA 3-0 AFRICAN LYON Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top