• HABARI MPYA

    Wednesday, August 31, 2016

    YANGA WATUMIE AKILI ZAO WENYEWE, WASIIAMINI SANA TFF

    LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ilianza wiki iliyopita na mwishoni mwa wiki mchezaji mwenye utata katika usajili wake, Hassan Ramadhani Kessy akaichezea klabu mpya, Yanga SC.
    Kessy alimaliza Mkataba wake Simba SC Juni 15, mwaka huu, lakini mapema Mei 25 aliinuliwa mkono kwa pamoja na Juma Mahadhi aliyesajiliwa kutoka Coastal Union kutambulishwa kwa mashabiki wa Yanga Uwanja wa Taifa.
    Aliyewainua mikono wachezaji hao wawili alikuwa ni Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga, Jerry Muro kabla ya mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation Cup (ASFC).
    Na wachezaji wote waliinuliwa mikono wakiwa wamevalishwa jezi za Yanga siku hiyo timu hiyo ikiwafunga Azam FC 3-1 na kubeba Kombe la ASFC.
    Siku chache baadaye, kabla ya Juni 15 Kessy akaanza mazoezi na Yanga SC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kujiandaa na mchezo wa kwanza wa Kundi A Kombe la Shirikisho dhidi ya MO Bejaia nchini Algeria.
    Na Yanga ikapaleka TFF orodha ya wachezaji wapya wa kuongeza kwenye Kombe la Shirikisho, akiwemo Kessy na kabla ya Juni 15 CAF ikatuma leseni za wachezaji hao Dar es Salaam.
    Kessy akaenda kambini nchini Uturuki na Yanga kwa wiki moja kabla ya timu kuingia Algeria siku mbili kabla ya mchezo ambao Yanga ilifungwa 1-0 Juni 19.
    Takriban saa 48 kabla ya mchezo huo wa kwanza Juni 19, zikatoka taarifa kwamba CAF inataka uthibitisho wa barua ya Simba SC kumruhusu Kessy kuichezea Yanga.
    Yanga hawakuwa na barua na hawakuweza kwenda kuiomba Simba SC, jambo ambalo likamfanya Kessy akose mechi zote za Kombe la Shirikisho hadi sasa. 
    Hatimaye Kessy akaichezea Yanga kwa mara ya kwanza mechi ya mashindnao Agosti 17, ikifungwa kwa penalti 4-1 na Azam FC baada ya sare ya 2-2 katika mchezo wa Ngao ya Jamii.
    Mchezo huo ni wa mashindano ya siku moja na matokeo yake umuhimu wake ni wa siku moja tu, hivyo sana Yanga hata kama ingeshinda ingepokonywa ushindi baadaye kwa kumchezesha Kessy kinyume cha sharia.
    Na siku moja kabla ya Ligi Kuu kuanza, TFF wakatoa taarifa isemayo; “Kamati ya Sheria na Hadhi za wachezaji imepitisha usajili wa wachezaji wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara huku ikiwa imepitisha jina la Hassan Ramadhani ‘Kessy’ kuitumikia Yanga SC kuanzia msimu huu 2016/17 baada ya kuona kuwa hana tatizo katika usajili, badala yake madai ambayo pande husika zinaweza kudaiana wakati mchezaji anaendeleza kipaji chake.
    Kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake, Richard Sinamtwa imepitia usajili wa timu zote na kujiridhisha kwamba suala la mchezaji Hassan Kessy limeegemea kwenye madai na si usajili ambako Simba ndiye mdai kwa kumtuhumu mchezaji huyo kuwa alianza kuitumikia Yanga kabla ya kumaliza mkataba wake Simba SC. Mkataba wake ulifika mwisho, Juni 15, 2016.
    Kama ni madai Simba inaweza kuendelea kumdai Kessy au Yanga SC wakati mchezaji huyo anatumika uwanjani kwa mwajiri mpya. 
    TFF inafuatilia na kuangalia haki ya Simba namna ya kupata haki yake baada ya kuwasilisha madai kuhusu kuvunja mkataba na mwajiri wake wa zamani.
    Kanuni hazimzuii mchezaji kuendelea kucheza kwa hoja ya madai badala yake suala hilo linaweza kumalizwa wakati mashindano yanaendelea. Kamati inaendelea kupitia malalamiko na pingamizi za wachezaji wengine na inatarajiwa kutoa taarifa rasmi kuhusu wachezaji wote wakati wowote kuanzia sasa,”. Mwisho wa taarifa ya TFF.
    Katika kesi mbili zinazofanana kabisa, ya Bokungu na Kessy kwa nini kuwe na majibu tofauti?
    Awali ya yote, ni TFF wanastahili lawama kwa kuthubutu kupokea jina la Kessy na kulituma CAF wakijua fika mchezaji huyo bado yupo ndani ya Mkataba na Simba.
    Wameipa Simba ushahidi na nguvu ya kisheria ya kufungua madai dhidi ya mchezaji Kessy kuvunja nao Mkataba kinyume cha sheria.
    Wazi hapa, Yanga wakithubutu kumtumia Kessy kabla ya kumalizana na Simba watafanya makosa na wapinzani wao hao wakienda kushitaki FIFA mambo yatakuwa mazito.
    Meneja wa Kessy, Athumani Tippo anaamini Mkataba wa kijana wake na Simba uliisha Juni 17 na beki huyo wa kulia akasaini Yanga SC Juni 21, baada ya kuzungumzo ya awali kufanyika mwishoni mwa Mei.   
    Lakini ushahidi unaonyesha kabla ya Juni 15, Kessy alikwishaanza kazi Yanga na alifanya mazoezi Uwanja wa Taifa na baadaye Uturuki. Hii pekee inamfunga Kessy kwamba alivunja Mkataba na Simba.
    Na Simba katika Mkataba wao na Kessy wameweka kipengele kinachosema mchezaji anapotaka kuvunja Mkataba anatakiwa kuilipa klabu dola 600,000 zaidi ya Sh. Bilioni 1.2 za Tanzania.
    Yanga wanatakiwa kujua wazi, Kessy ni bomu ambalo wakiliingiza uwanjani litawalipukia. Kessy atawaponza Yanga wapokonywe pointi zote iwapo tu watamtumia kabla ya kumalizana na Simba.
    Suala la Kessy halina tofauti sana na suala la  aliyekuwa beki wa TP Mazembe ya DRC, Janvier Besala Bokungu ambaye bahati nzuri kwa sasa yuko Simba SC.
    Beki huyo raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) amewahi kuiponza TP Mazembe ya DRC ikaondolewa kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika licha ya kufuzu mwaka 2011 kwa kuzitoa Simba SC ya Tanzania na Wydad Casablanca ya Morocco.
    TP Mazembe iliifunga Simba SC 3-1 mjini Lubumbashi na 3-2 Dar es Salaam katika hatua ya 32 Bora, kabla ya kwenda kuitoa Wydad Casablanca katika 16 Bora na kufuzu hatua ya makundi.
    Hata hivyo, Simba ilirudishwa mashindanoni baada ya kushinda rufaa waliyomkatia beki wa Mazembe, Janvier Besala Bokungu, aliyevunja mkataba kinyume cha taratibu na klabu ya Esperance ya Tunisia.
    Bokongu alimaliza msimu Tunisia, lakini akaenda kusaini Mazembe akiwa amebakiza siku chache kumaliza Mkataba wake Esperance.
    Shirikisho la Soka DRC na la Afrika (CAF) yote yakamuidhinisha Bokungu kuichezea Mazembe na kumpa leseni hata akacheza dhidi ya Simba SC.
    Lakini Esperance kwa kuikomoa Mazembe, wakaipa siri hiyo Simba SC ambayo ilikata rufaa CAF na kushinda hatimaye kurejeshwa kwenye mashindano  na ikacheza mechi ya mkondo mmoja na Wydad Casablanca mjini Cairo, Misri na kufungwa 3-0, hivyo kuangukia kwenye hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho Afrika, ambako ilitolewa na DC Motema Pembe ya DRC kwa mabao 2-1.
    Utaona Bokungu alikuwa ana leseni ya CAF ya kumruhusu kucheza mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini haikuisaidia Mazembe kuepuka kuenguliwa kwenye mashindano mwaka 2012.
    Na hata Yanga walimtumia Kessy kwenye mchezo wao wa kwanza wa Ligi Kuu wakishinda 3-0 dhidi ya African Lyon kwa sababu ana leseni ya TFF, wenye ligi yao.
    Lakini Yanga wajue kwamba hata Bokungu alikuwa ana leseni ya CAF wenye mashindano yao ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ingawa haikusaidia Mazembe kuepuka kuenguliwa mashindanodni. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA WATUMIE AKILI ZAO WENYEWE, WASIIAMINI SANA TFF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top