• HABARI MPYA

    Friday, August 26, 2016

    KILA LA HERI TIMU YA SOKA LA UFUKWENI TANZANIA, YAMENYANA NA IVORY COAST LEO

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MCHEZO wa kwanza wa mpira wa miguu wa ufukweni, kati ya Tanzania na Ivory Coast unatarajiwa kufanyika kesho kuanzia saa 10.00 jioni kwenye Uwanja uliotengenezwa maalumu kwa ajili ya mchezo huo kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Ilala jijini Dar es Salaam.
    Tanzania imepania kufanya vema dhidi ya Ivory Coast iliyoingia Dar es Salaam, usiku wa kuamkia Jumanne kwa ajili ya mchezo huo wa kwanza wa kuwania nafasi ya kucheza Kombe la Mataifa ya Afrika ambako fainali zake zitafanyika Lagos, Nigeria.
    Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Ali Sharif ‘Adolph’, licha ya kupania mchezo huo, anakiri anakutana na timu ngumu ambayo inashika nafasi ya pili barani Afrika, lakini watatumia uzoefu kupata ushindi ili kuweka historia katika mchezo huo nchini.
    Mchezo huo utakaochezeshwa na waamuzi kutoka Uganda ambao ni Shafic Mugerwa atakayepuliza kipyenga na wasaidizi wake ni Ivan Bayige Kintu na Muhammad Ssenteza, Mtunza muda atakuwa Adil Ouchker wa Morocco huku Kamishna akiwa ni Reverien Ndikuriyo wa Burundi.
    Timu hizo zinatarajiwa kucheza mechi mbili za kuwania kufuzu kwani mara baada ya mchezo wa Dar es Salaam, zitarudiana tena Ivory Coast na mshindi wa jumla atakuwa amefanikiwa kufuzu kwa fainali.
    Kwa upande wa Tanzania, Kocha Mkuu wa timu hiyo, John Mwansasu, anaendelea na mazoezi na wachezaji wake 16 aliowatangaza wiki iliyopita. Kikosi hicho kinaundwa na wachezaji sita kutoka Zanzibar na 10 Tanzania Bara.
    Wanaounda kikosi hicho ni Talib Ame, Ahamada, Mohammed Makame, Ahamed Rajab (golikipa) Khamis Said na Yacob Mohamed wote kutoka Zanzibar. Wengine ni Ally Raby, Mwalimu Akida, Khalifa Mgaya, Rolland Revocatus, Juma Sultan, Rajab Ghana, Samwel Salonge, Kashiru Salum, Juma Juma na Kevin Baraka.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KILA LA HERI TIMU YA SOKA LA UFUKWENI TANZANIA, YAMENYANA NA IVORY COAST LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top