• HABARI MPYA

  Tuesday, August 09, 2016

  SIMBA HII NI MWISHO WA MATATIZO- MAVUGO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI mpya wa Simba SC, Laudit Mavugo amesema kwamba sasa yupo katika timu nzuri zaidi maishani mwake.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE jana baada ya kuisaidia Simba SC kushinda 4-0 dhidi ya AFC Leopard ya Kenya kwenye mchezo wa kirafiki, Mavugo alisema kwamba amefurahia mwanzo mzuri katika timu ya Msimbazi.
  “Nimefurahi, nimekuwa na mwanzo mzuri katika timu, nimetokea benchi nimekwenda kufunga na zaidi timu imecheza vizuri sana, naweza kusema hii ni timu nzuri zaidi kwangu kuwahi kuchezea,”alisema.
  Mavugo akishangilia kwa kumbeba Shizza Kichuya jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
  Mavugo anayetokea Vital’O ya kwao, alisema kwamba sasa anaelekeza nguvu zake katika kuisaidia Simba SC kushinda mataji. “Kwa ushirikiano na wachezaji wenzangu naamini tutaweza, tuna timu nzuri,”alisema. 
  Simba SC jana ilkisherehekea vyema miaka 80 jioni ya leo baada ya kuifunga AFC Leopard ya Kenya mabao 4-0 katika mchezo wa kirafiki Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Mshambuliaji chipukizi wa kimataifa wa Tanzania, Ibrahim Hajib Migomba aliendelea kumvutia kocha mpya, Mcameroon Joseph Marius Omog baada ya kufunga mabao mawili, huku wachezaji wapya, Mrundi Laudit Mavugo na Shizza Kichuya wakifunga pia. 
  Hadi mapumziko, Simba walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa na Hajib dakika ya 38 kwa shuti la umbali wa mita takriban 30 baada ya kupokea pasi ya kiungo Mkongo, Mussa Ndusha.
  Mabadliko ya karibu nusu kikosi yaliyofanywa na kocha Omog, anayesaidiwa na Mganda, Jackson Mayanja kipindi cha pili yaliisaidia Simba kupata mabao matatu.
  Hajib alimalizia vizuri krosi ya Kichuya kuifungia Simba SC bao la pili dakika ya 56 na dakika 58 Jamal Mnyate akapoteza nafasi nzuri aliyotengenezewa na Mavungo.
  Lakini Kichuya akawainua vitini mashabiki wa Simba SC walioongozwa na Rais wa klabu, Evans Elieza Aveva na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwa kufunga bao la tatu dakika ya 66, akimalizia krosi ya Mavugo.
  Mavugo aliyejiunga na Simba SC mwishoni mwa wiki, akaifungia Simba SC bao la nne dakika ya 82 akiunganisha krosi nzuri ya Kichuya, aliyekuwa nyota wa mchezo wa leo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA HII NI MWISHO WA MATATIZO- MAVUGO Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top