• HABARI MPYA

  Sunday, January 17, 2016

  YANGA SC YAREJEA KILELENI LIGI KUU, YAILAZA 1-0 NDANDA FC, TAMBWE AKOSA PENALTI TAIFA

  RATIBA LIGI KUU YA VODACOM TZ BARA;
  Januari 17, 2016
  Yanga SC 1-0 Ndanda FC
  Januari 16, 2016
  Azam FC Vs African Sports 
  Simba SC 1-0 Mtibwa Sugar
  JKT Ruvu 1-5 Mgambo JKT
  Toto Africans 0-1 Prisons
  Stand United 1-0 Kagera Sugar
  Mbeya City 1-0 Mwadui FC
  Coastal Union 1-1 Majimaji
  Kocha wa Yanga SC, Mholanzi Hans van der Pluijm akimpongeza Nahodha wake, Kevin Yondan baada ya mechi leo Uwanja wa Taifa

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  YANGA SC imefanikiwa kurejea kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kufuatia ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ndanda FC ya Mtwara jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Ahsante kwake mfungaji wa bao hilo pekee, Kevin Patrick Yondan kwa mkwaju wa penalti kipindi cha pili na sasa Yanga SC inafikisha pointi 36 baada ya kucheza mechi 14, ikilingana na Azam FC wanaoangukia nafasi ya pili.
  Yanga SC sasa wanakaa kileleni mwa Ligi Kuu kwa wastani wa mabao tu, wakiwa wamefunga mabao 31 na kufungwa matano, wakati Azam FC imefunga mabao 28 na kufungwa tisa.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Mathew Akrama wa Mwanza, Yanga SC walitawala zaidi kipindi cha kwanza na kupoteza nafasi kadhaa za kufunga mabao.
  Yanga SC walipoteza nafasi nzuri ya kufunga dakika ya 29, baada ya shuti la mpira wa adhabu la beki wake wa kulia, Juma Abdul kupanguliwa vizuri na kipa Jeremiah Kisubi wa Ndanda.
  Yanga SC walisukuma shambulizi kali langoni mwa Ndanda dakika ya 42 na kuzua kizaaa, kabla ya beki mmoja kuokoa mpira uliokuwa unaelekea nyavuni.
  Kipindi cha pili, Yanga SC walirudi kwa kasi ile ile ya mashambulizi na kufanikiwa kupata penalti dakika ya 47, baada ya beki wa Ndanda, Paul Ngalema kumuangusha winga Simon Msuva kwenye boksi. 
  Hata hivyo, mshambuliaji Mrundi Amissi Tambwe akaenda kugongesha mwamba wa juu mkwaju wake na ingawa alijaribu kuucheza tena uliporudi uwanjani, hakufanikiwa.

  Kikosi cha Yanga SC kilichoifunga Ndanda FC 1-0 leo Uwanja wa Taifa
  Lakini Yanga SC wakafanikiwa kupata bao kwa penalti nyingine dakika ya 60 kupitia kwa Nahodha wake wa leo, Kevin Yondan kufuatia kiungo Deus Kaseke kuangushwa na Hemed Khoja aliyemkwatua kwa nyuma.
  Kaseke hakuweza kuendelea na mchezo baada ya rafu hiyo na nafasi yake kuchukuliwa na Issoufou Boubacar dakika ya 67.
  Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Deogratius Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Vincent Bossou, Kelvin Yondan, Salum Telela, Simon Msuva, Thabani Kamusoko, Donald Ngoma, Amissi Tambwe/Malimi Busungu dk71 na Deus Kaseke/Issoufou Boubacar dk67.
  Ndanda FC: Jeremiah Kisubi, Azizi Sibo, Paul Ngalema, Kassian Ponera, Salvatory Ntebe, Jackson Nkwera/Omega Seme dk39, William Lucian ‘Gallas’, Hemed Khoja, Atupele Green, Kiggi Makassy/Masoud Ally dk71 na Brison Raphael.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA SC YAREJEA KILELENI LIGI KUU, YAILAZA 1-0 NDANDA FC, TAMBWE AKOSA PENALTI TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top