• HABARI MPYA

    Sunday, January 17, 2016

    NIYONZIMA AOMBA MSAMAHA YANGA, JANGWANI WALAINIKA, HUENDA KIJANA AKAREJESHWA KUNDINI MUDA SI MREFU

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KIUNGO Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima ameomba msamaha Yanga SC na kuahidi kutorudia kuikwaza klabu kwa namna yoyote.
    Mwezi uliopita, Yanga SC ilitangaza kuvunja Mkataba na Nahodha huyo wa Rwanda kwa tuhuma za kukiuka vipengele vya Mkataba wake.
    Lakini leo katika Mkutano na Waandishi wa Habari makao makuu ya klabu, Jangwani, Dar es Salaam, Niyonzima ameomba msamaha ili arejeshwe kundini.
    “Ninapenda kuchukua fursa hii kuomba msamaha kwa uongozi, benchi la ufundi na wachezaji wenzangu pamoja na wanachama na wapenzi. Ninaipenda timu yangu na ninapenda kuendelea kuitumikia,”amesema.
    Haruna Niyonzima (kulia) akizungumza na Waandishi wa Habari leo makao makuu ya klabu, Jangwani, Dar es Salaam. Kushoto ni Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga SC, Jerry Muro

    Aidha, Niyonzima amesema kwamba kulitokea kutoelewana kimawasiliano na ofisi ya Katibu Mkuu, Dk Jonas Tiboroha kiasi cha kulifikisha suala hilo kwenye hatua hiyo.
    Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga SC, Jerry Muro amesema kwamba suala la Niyonzima limefika katika uongozi mkuu wa klabu na lipo katika hatua nzuri.
    Ingawa Muro hakuweza wazi, lakini inavyoonekana muda si mrefu Yanga itatangaza kuzika tofauti zake na mchezaji huyo na kumrejesha kundini rasmi.  
    Yanga SC ilitangaza kuvunja Mkataba na Niyonzima, baada ya kuchelewa kurejea klabuni kufuatia kuruhusiwa kwenda kuichezea Rwanda katika Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki, CECAFA Challenge nchini Ethiopia Novemba.
    Awali, Yanga SC ilimsimamisha kwa muda usiojulikana Niyonzima kabla ya suala lake kupelekwa Kamati ya Nidhamu, ambayo hatimaye ilichukua maamuzi magumu.
    Niyonzima (katikati) akiwa na viungo wenzake, Mzimbabwe Thabani Kamusoko (kulia) na Mkongo Mbuyu Twite (kushoto). Watatu hao huenda wakaanza kucheza pamoja tena muda si mrefu
    Pamoja na Niyonzima kuwasilisha vielelezo vyote vya kumsafisha, lakini uchunguzi wa Kamati ya Nidhamu ulijiaminisha kiungo huyo alidanganya ili kukwepa hatua za kinidhamu.  
    Ulibaini plasta gumu (PoP) alilofunga baada ya kurejea akiwa amechelewa ilikuwa ni ‘geresha’ na vielelezo vingine alivyowasilisha vilikuwa ‘feki’ pia.
    Na ikamnasa kwenye picha za video siku za karibuni ‘akijirusha’ sehemu mbalimbali za starehe ikiwemo kwenye onyesho la mwanamuziki Ali Kiba.
    Haruna aliyezaliwa Februari 5, mwaka 1990 Gisenyi nchini Rwanda, alijiunga na Yanga SC mwaka 2011 akitokea APR ya kwao, ambako aliwasili mwaka 2007 akitokea Rayon aliyoichezea kwa misimu miwili baada ya kujiunga nayo akitokea Etincelles iliyomuibua mwaka 2005.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NIYONZIMA AOMBA MSAMAHA YANGA, JANGWANI WALAINIKA, HUENDA KIJANA AKAREJESHWA KUNDINI MUDA SI MREFU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top