• HABARI MPYA

  Sunday, January 10, 2016

  YANGA SC NAO NJE, WANG’OLEWA KWA MATUTA NA URA

  Na Prince Akbar, ZANZIBAR
  YANGA SC imeaga michuano ya Kombe la Mapinduzi baada ya kufungwa na URA ya Uganda kwa penalti 4-3, kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 90.
  Penalti za Yanga zilifungwa na Kevin Yondan, Deo Munishi ‘Dida’ na Simon Msuva huku Malimi Busungu na Geoffrey Mwashiuya wakikosa, wakati za URA zimefungwa na Deo Othieno, Said Kyeyune, Jimmy Kulaba na Brian Bwete, wakati Sam Sekito alikosa.
  Awali ndani ya dakika 90, Yanga SC walikuwa wa kwanza kupata bao lililofungwa na mshambuliaji Mrundi, Amissi Joselyn Tambwe.
  Tambwe alifunga bao hilo dakika ya 13 kwa kichwa akimalizia mpira uliorudi baada ya kutemwa na kipa wa URA, Brian Bwete kufuatia mchomo wa winga Simon Msuva.
  Yanga ingeweza kumaliza dakika 45 za kwanza inaongoza kwa mabao zaidi kama si wachezaji wake kupoteza nafasi za wazi.
  Mshambuliaji wa Yanga SC, Amissi Tambwe akiwatoka wachezaji wa URA usiku wa leo Uwanja wa Amaan
  Winga wa Yanga SC, SImon Msuva akimiliki mpira mbele ya beki wa URA, Allan Munaaba

  Mshambuliaji Donald Ngoma akiwa karibu na kipa wa URA, Brian Bwete katika mastaajabu ya wengi alipiga juu na kuharibu krosi nzuri ya Msuva dakika ya 15.
  URA nao walipoteza nafasi dakika ya 18 kupitia kwa mshambuliaji wao, Elkannah Nkugwa aliyepiga pembeni mpira na kuharibu pasi aliyopewa na Said Kyeyune.
  Kipa wa URA aliinyima tena Yanga nafasi ya kufunga baada ya kudaka shuti lililopigwa na Tambwe aliyemalizia pasi ya kiungo stadi, Thabani Kamusoko dakika ya 38.
  Kipindi cha pili, URA walikuja kivingine na kufanikiwa kusawazisha bao hilo kupitia kwa Peter Lwasa dakika ya Dk 76 baada ya makosa ya safu ya ulinzi ya Yanga.
  Baada ya bao, hilo Yanga SC waliongeza kasi ya mashambulizi kwenye lango la URA kusaka ushindi, lakini hawakufanikiwa hadi walipokwenda kufia kwenye mikwaju ya penalti.
  URA sasa itakutana na Mtibwa Sugar iliyoitoa Simba SC kwa kuifunga bao 1-0 katika fainali Jumatano Uwanja wa Amaan, wakati Yanga inarejea Dar es Salaam.
  Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Mwinyi Mngwali, Kevin Yondan, Vincent Bossou, Mbuyu Twite/Salum Telela dk79, Simon Msuva, Thabani Kamusoko, Donald Ngoma/Malimi Busungu dk75, Amissi Tambwe/Paul Nonga dk87 na Deus Kaseke/Geofrey Mwashiuya dk69.
  URA FC; Brian Bwete, Simon Massa/Peter Lwasa dk63, Alan Munaaba, Jimmy Kulaba, Sam Senkoom, Osvcar Agaba, Julius Ntambi/Deo Otieno dk84, Said Kyeyune, Derick Tekwo/Shaffi Kagima dk32, Villa Oramuchani/Sam Sekito dk63 na Elkannah Nkugwa.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA SC NAO NJE, WANG’OLEWA KWA MATUTA NA URA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top