• HABARI MPYA

    Sunday, January 10, 2016

    SIMBA SC ASUBUHI TU KESHO WAPO WAR, WAGONGWA 1-0 NA MTIBWA SUGAR

    Na Princess Asia, ZANZIBAR
    SIMBA SC imevuliwa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi, baada ya kufungwa bao 1-0 na Mtibwa Sugar katika mchezo wa Nusu Fainali uliofanyika Uwanja wa Amaan, Zanzibar jioni ya leo.
    Shujaa wa Mtibwa Sugar FC leo alikuwa ni kiungo Ibrahim Rajab ‘Jeba’ aliyefunga bao hilo pekee dakika ya 45 akimalizia mpira uliopanguliwa na kipa Peter Manyika baada ya shuti la mshambuliaji Hussein Javu anayecheza kwa mkopo kutoka Yanga SC.
    Pamoja na kufungwa, Simba SC walicheza vizuri wakiongozwa na mkongwe Mussa Hassan Mgosi ingawa bahati haikuwa yao.
    Nafasi nzuri zaidi alipoteza Mwinyi Kazimoto dakika ya 42, ambaye pamoja na kuwatoka vizuri mabeki wa Mtibwa Sugar baada ya pasi ya Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, lakini wakati anakwenda kufunga kipa Said Mohamed akawahi kutokea na kudaka.
    Ibrahim Rajab Jeba (kulia) akishangilia na wenzake baada ya kufunga

    Dakika ya 11 Mussa Hassan Mgosi akiwa ndani ya 18 alichelewa kuunganisha krosi ya Mwinyi Kazimoto na kumpa nafasi beki wa Mtibwa Sugar, Dickson Daudi kuokoa hatari hiyo langoni mwao.
    Mtibwa Sugar walijibu shambulio hilo katika dakika ya 22, lakini Jeba akiwa amebaki na kipa akapiga nje na kupoteza krosi nzuri iliyopigwa na Ally Shomary.
    Dakika ya 30 Mussa Hassani Mgosi alipiga kichwa fyongo na kumfanya kipa wa Mtibwa Sugar Said Mohammed adake kiurahisi.
    Manyika aliruka na kuwahi kupangua shuti la Shizza Kichuya aliyepata krosi ya Mohammed Ibrahim na kuinyima Mtibwa Sugar nafasi ya kufunga.
    Kipindi cha pili, kocha Muingereza wa Simba SC, Dylan Kerr alianza na kupangua kikosi akiwapumzisha beki Emery Nimubona, kiungo Awadh Juma na mshambuliaji Mussa Mgosi na nafasi zao kuchukuliwa na Brian Majwega, Said Ndemla na Ibrahim Hajib.
    Hata hivyo, Mtibwa Sugar waliendelea kulitia misukouko lango la SImba na dakika ya 56 kipa Peter Manyika aliokoa kwa ustadi mkubwa mpira wa Kichuya na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.
    Kipa Said Mohammed wa Mtibwa Sugar (kulia) akiwa amedaka mpira wa Mwinyi Kazimoto aliyeruka juu
    Mussa Mgosi wa Simba SC (kulia) akimtoka Shizza Kichuya wa Mtibwa Sugar
    Mfungaji wa bao pekee la Mtibwa, Ibrahim Jeba (kushoto) akimtoka beki wa Simba, Mohammed Hussein 'Tshabalala'

    Dakika ya 66 Danny Lyanga aliunganishia nje krosi maridadi ya Tshabalala na dakika ya 90, Abdi Banda akiwa ndani ya 18 alipiga shuti kali, lakini kipa Said Mohammed akatema kabla ya kuurukia na kuudaka.
    Kwa matokeo hayo, Simba SC watapanda boti kesho mapema asubuhi kurejea Dar ea Salaam, wakati Mtibwa Sugar itasubiri mshindi kati ya Yanga SC na URA ya Uganda usiku wa leo, ikutane naye katika Fainali Jumatano.
    Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Peter Manyika, Emery Nimuboma/Brian Majwega dk46, Mohammed Hussein 'Tshabalala', Hassan Isihaka, Juuko Murshid, Justice Majabvi, Awadh Juma/Said Ndemla dk46, Jonas Mkude, Mussa Mgosi/Ibrahim Hajib dk46, Danny Lyanga/Paul Kiongera dk76 na Mwinyi Kazimoto/Abdi Banda dk86.
    Mtibwa Sugar; Said Mohammed, Shaaban Nditi, Ally Shomary, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Dickson Daudi, Salim Mbonde, Mohammed Ibrahim, Muzammil Yassin, Hussein Javu/Jaffar Salum dk68, Ibrahim Rajab ‘Jeba’/Vincent Barnabas dk80 na Shiza Kichuya.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC ASUBUHI TU KESHO WAPO WAR, WAGONGWA 1-0 NA MTIBWA SUGAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top