• HABARI MPYA

    Saturday, January 16, 2016

    KIPUTE CHA AZAM FC NA AFRICAN SPORTS NI USIKU LEO CHAMAZI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MECHI ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kati ya vinara, Azam FC na African Sports ya Tanga itachezwa kuanzia Saa 1:00 usiku Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
    Leo kutakuwa na jumla ya mechi tatu za Ligi Kuu, Dar es Salaam, moja Uwanja wa Karume kati ya JKT Ruvu na JKT Mgambo na nyingine Uwanja wa Taifa, kati ya Simba SC na Mtibwa Sugar.
    Na ili kuwapa fursa watu kuona mechi zote mbili kubwa za leo kupitia Azam TV, ndiyo maana mchezo mmoja wa Dar es Salaam umepelekwa usiku.
    Ikumbukwe Azam FC iliyo kileleni mwa Ligi Kuu kwa pointi zake 35 baada ya kucheza mechi 13, ikifuatiwa na mabingwa watetezi, Yanga SC wenye pointi 33 za mechi 13 pia, imepania kushinda mechi hiyo ili kuzidi kupiga kasi katika mbio za ubingwa.

    Baada tu ya kutolewa katika Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar wiki iliyopita, Azam FC ilirejea Dar es Salaam mapema kuanza maandalizi ya mechi dhidi ya Sports.
    Na katika kipindi hiki kifupi wamefanya hadi mazoezi ya ufukweni kuhakikisha wachezaji wake wanakuwa fiti kikamilifu.  
    Mechi nyingine za Ligi Kuu leo ni baina ya mabingwa wa zamani wa ligi hiyo, Simba SC na Mtibwa Sugar Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia Saa 10:00 jioni.
    Mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu, wanakutana Jumamosi ya leo ikiwa ni wiki moja tangu wakutane katika Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar, Mtibwa Sugar ikiilaza Simba SC 1-0, bao pekee la Ibrahim Rajab ‘Jeba’.
    Na baada ya kipigo hicho, Simba SC iliwafukuza makocha wake, Muingereza, Dylan Kerr na Mkenya Iddi Salim na sasa Mganda, Jackson Mayanja ndiye yupo na timu.
    Mtibwa Sugar nao wataingia katika mchezo wa kesho wakiwa na kumbukumbu ya kufungwa mabao 3-1 na URA ya Uganda katika fainali ya Kombe la Mapinduzi Jumatano. 
    Mechi nyingine za ligi hiyo leo ni kati ya JKT Ruvu na Mgambo JKT Uwanja wa Karume, Dar es Salaam, Toto Africans na Prisons Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Stand United na Kagera Sugar Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, Mbeya City na Mwadui FC Uwanja wa Sokoine, Mbeya na Coastal Union na Majimaji wa Uwanja wa Majimaji, Songea.
    Ligi Kuu itaendelea kesho kwa mechi moja tu, mabingwa watetezi, Yanga SCwakiikaribisha Ndanda FC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Yanga SC nayo inarejea kwenye Ligi Kuu baada ya kutolewa katika Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi, wakifungwa kwa penalti 4-3 na URA kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 90.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KIPUTE CHA AZAM FC NA AFRICAN SPORTS NI USIKU LEO CHAMAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top