• HABARI MPYA

  Monday, January 18, 2016

  CANNAVARO AKABIDHIWA ‘SILAHA MPYA’ KUKOMBOA NAMBA YAKE KWA BOSSOU

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  NAHODHA wa Yanga SC, Nadir Haroub Ali ‘Cannavaro’ leo amekabidhiwa vifaa vipya vya michezo tayari kuanza mazoezi kufuatia kupona maumivu ya mguu.
  Cannavaro amekuwa nje tangu Novemba 17 mwaka jana alipoumia akiichezea timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars katika mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya wenyeji, Algeria mjini Blida.
  Na baada ya vipimo vya mwisho juzi kuthibitisha anaweza kuanza mazoezi mepesi, leo Cannavaro amewasili makao makuu ya klabu, Jangwani, Dar es Salaam kuchukua vifaa.
  Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga SC, Jerry Muro amesema kwamba Cannavaro amefika makao makuu ya klabu leo kuchukua vifaa vipya vya mazoezi.
  Na Muro amesema hizo ni habari njema kwa klabu katika wakati huu ambao vita ya ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara imepamba moto.
  Cannavaro (kulia) akiwa na Jerry Muro baada ya kukabidhiwa vifaa vya mazoezi
  Cannavaro akiwa amekumbatia vifaa vyake makao makuu ya klabu, Jangwani leo

  “NI habari njema kumpokea tena Nahodha wetu, Cannavaro ambaye alikuwa nje kwa muda mrefu kutokana na majeruhi. Tunatarajia kesho ataanza mazoezi mepesi,”amesema Muro.
  Yanga SC jana imefanikiwa kurejea kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kufuatia ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ndanda FC ya Mtwara Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Ahsante kwake mfungaji wa bao hilo pekee, Kevin Patrick Yondan kwa mkwaju wa penalti kipindi cha pili na sasa Yanga SC inafikisha pointi 36 baada ya kucheza mechi 14, ikilingana na Azam FC wanaoangukia nafasi ya pili.
  Vincent Bossou kwa sasa anafanya kazi nzuri katika nafasi ya Cannavaro

  Yanga SC sasa wanakaa kileleni mwa Ligi Kuu kwa wastani wa mabao tu, wakiwa wamefunga mabao 31 na kufungwa matano, wakati Azam FC imefunga mabao 28 na kufungwa tisa.
  Hata hivyo, baada ya kupona Cannavaro atalazimika kupambana kurudi katika kikosi cha kwanza kutokana na beki Mtogo, Vincent Bossou aliyekuwa anashika nafasi yake kufanya vizuri.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: CANNAVARO AKABIDHIWA ‘SILAHA MPYA’ KUKOMBOA NAMBA YAKE KWA BOSSOU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top