• HABARI MPYA

  Saturday, January 16, 2016

  AZAM FC YANG’ANG’ANIWA NA AFRICAN SPORTS, SARE 1-1 CHAMAZI

  RATIBA LIGI KUU YA VODACOM TZ BARA;
  Januari 16, 2016
  Azam FC 1-1 African Sports 
  Simba SC 1-0 Mtibwa Sugar
  JKT Ruvu 1-5 Mgambo JKT
  Toto Africans 0-1 Prisons
  Stand United 1-0 Kagera Sugar
  Mbeya City 1-0 Mwadui FC
  Coastal Union 1-1 Majimaji
  Kesho; Januari 17, 2016
  Yanga SC Vs Ndanda FC
  Wachezaji wa Azam FC wakimpongeza mwenzao, Frank Domayo baada ya kufunga leo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam

  AZAM FC imelazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na African Sports ya Tanga katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara usiku huu Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
  Sare hiyo inaiongezea Azam FC pointi moja na kufikisha 36 baada ya mechi 14, ikiwazidi pointi tatu mabingwa watetezi, Yanga SC walio katika nafasi ya pili, ingawa wana mechi moja mkononi.
  Katika mchezo uliochezeshwa na refa Jonesia Rukyaa wa Kagera aliyesaidiwa na Ferdinand Chacha na Julius Kasitu, hadi mapumziko Azam FC walikuwa mbele kwa bao 1-0.
  Bao hilo lilifungwa na kiungo wa zamani wa Yanga SC, Frank Raymond Domayo dakika ya 28 kwa shuti la umbali wa takriban mita 20, baada ya kupokea pasi ya Nahodha John Raphael Bocco.
  Pamoja na kumaliza dakika 45 za kwanza, wakiwa nyuma, lakini African Sports walionyesha upinzani kwa Azam FC na mara mbili walikaribia kupata bao.
  Kipindi cha pili, Sports iliyo chini ya kocha wa zamani wa Simba SC, Ramadhani Aluko iliongeza bidii na kufanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 59 kupitia kwa Hamad Mbumba aliyemalizia mpira wa adhabu uliopigwa na Mwaita Gereza.
  Baada ya bao hilo, timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu na kosakosa zilikuwa za pande zote mbili.
  Matokeo hayo yanaipunguza kasi Azam FC katika mbio za ubingwa na sasa, mabingwa watetezi, Yanga SC wanaweza kurejea kileleni iwapo watashinda dhidi ya Ndanda FC kesho.
  Kwa African Sports, sare hiyo ya ugenini inakuwa ahueni katika harakati zao za kujiepusha na balaa la kushuka daraja.
  Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Aishi Manula, Shomary Kapombe, Waziri Salum/Farid Mussa dk62, Abdallah Kheri, Serge Wawa, Erasto Nyoni, Jean Baptiste Mugiraneza, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, John Bocco ‘Adebayor’, Frank Domayo/Mudathir Yahya dk65 na Kipre Herman Tchetche.
  African Sports; Zakaria Mwaluko, Mwaita Gereza, Khalifa tweve, Rahim Juma, Juma Shemvuni, Ally Ramadhani/James Mendi dk86, Mussa Chambega, Pera Ramadhani, Hamad Nathaniel, Hassan Materema/Mohammed Mtindi dk47 na Rajab Isihaka/Hussein Issa dk70. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AZAM FC YANG’ANG’ANIWA NA AFRICAN SPORTS, SARE 1-1 CHAMAZI Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top