• HABARI MPYA

  Monday, January 18, 2016

  AYA 15 ZA SAID MDOE: UJUAJI ULIOKITHIRI SUMU YA MAENDELEO YA MUZIKI

  Zaidi ya miaka kumili iliyopita mwimbaji mkongwe wa muziki wa dansi, Hassan Rehani Bicthuka alisimamishwa kazi Msondo Ngoma baada ya kukataa kushiriki onyesho la pamoja dhidi ya The African Stars “Twanga Pepeta”. 
  Bicthuka alikataa kushiriki onyesho hilo lililofanyika Diamond Jubilee kwa madai kuwa hawezi kushindana na watoto wadogo. 
  Kipindi hicho Twanga Pepeta ilikuwa iko juu ile mbaya, nyimbo zake zilishika kila kona ya Tanzania, ilikuwa ni kama bendi ya kizazi kipya cha muziki wa dansi. 

  Kitendo cha Bicthuka kukataa kushiriki onyesho hilo hakikukubalika ambapo marehemu Muhidin Guromo licha ya uswahiba wake mkubwa na Bitchuka, akashiriki kumsimamisha na huo ndiyo ukawa mwanzo wa Bitchuka kurejea Sikinde. 
  Mwanamuziki wa kizazi kipya Inspector Haroun “Babu” aliwahi kuniambia kuwa siku moja alipanda jukwaa la Msondo Ngoma pale TCC Club akashiriki kuimba moja ya nyimbo maarufu za bendi hiyo lakini katikati ya wimbo akashushwa kwa agizo la Said Mabela. 
  Kisa cha kushushwa jukwaani kwa Inspector Haroun ni kwamba alikuwa hajui kuimba muziki wa dansi. 
  Hata kama ni kweli Inspector hajui kuimba muziki wa dansi, basi kwa heshima aliyonayo, alipaswa kutafutiwa njia inayolingana na heshima yake. Msanii wa kizazi kipya kwenda kuomba ‘lift’ kwenye jukwaa la dansi ni jambo lililostahili kufurahiwa badala ya kubezwa. 
  Nimeanzia mbali kuonyesha mifano michache kati ya mingi inayoonyesha namna wasanii wengi wa dansi walivyo na “u-mimi”- namna wanavyoamini kuwa wao wanajua kuliko yeyote yule. 
  Twanga ikaitwa bendi ya watoto, FM Academia iliwahi kuitwa bendi ya “wakuja” (sio wazawa), Akudo wakaitwa wazee wa ‘copy and paste’ – kwamba wanahamisha nyimbo za Kikongo kutoka kwenye lugha yao na kuzileta kwenye Kiswahili. 
  Yote hayo ni kuonyesha kuwa katika muziki wa dansi hakuna utamaduni wa kumkubali aliye juu, lazima atapigwa madongo, atapewa majina kadha wa kadha ili kumkatisha tamaa. 
  Leo Christian Bella anaitwa msanii wa bongo fleva, KWELI? Yaani mtu akifanya kolabo na wasanii wa bongo fleva basi anakuwa sio msanii wa dansi? 
  Nilidhani wanamuziki wa dansi wangejivunia mafanikio ya Bella na kuyachukulia kama darasa badala ya kuyakimbia kwa kivuli cha bongo fleva. 
  Hivi Bella ndio msanii wa kwanza kuimba pamoja na bongo fleva? King Kiki aliimba na Kwanza Unit na Mr II, Ally Chocky aliimba na Sister P, Zahir ally Zorro aliimba na Fid Q, Tarsis Masela aliimba na Chid Benz, Dk. Remmy aliimba na Mr II, Khalid Chokoraa aliimba na Banana mbona hao wote hawakuitwa wasanii wa bongo fleva? 
  Wanamuziki wa dansi na wadau wa kweli wa muziki wa dansi wapunguze ujuaji, wapunguze ubishi, wakubali kukosolewa, wakiri kuwa soko lao limeporomoka, wawaunge mkono wasanii wachache wanaofanya vizuri maana bila kuyakubali hayo basi hakuna namna, muziki wa dansi utazidi kudidimia. 
  Naendelea kusisitiza kwa mara nyingine tena kuwa wanamuziki wa dansi wana hazina kubwa ya ujuzi na uwezo hali ya juu, lakini kinachowaponza ni UJUAJI uliokithiri, ujuaji wa kuamini kuwa mtu pekee anayestahili kuwakosoa ni yule anayejua muziki huku wakisahau kuwa zaidi ya asilimia 80 ya wateja wao ni wale wasiojua ABC ya muziki lakini wamejaaliwa masikio ya kutambua kitu kizuri.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AYA 15 ZA SAID MDOE: UJUAJI ULIOKITHIRI SUMU YA MAENDELEO YA MUZIKI Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top