• HABARI MPYA

  Monday, September 22, 2014

  YANGA SC WAPEWA SHARTI MOJA TU WAKITEKELEZA WANALAMBA MILIONI 155

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  YANGA SC wamepewa sharti moja tu na Bodi ya Ligi, ambalo wakitekeleza watapatiwa Sh. Milioni 155.
  Sharti gani hilo? Msimu uliopita Yanga SC walisusia fedha za haki ya matangazo ya Televisheni ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara zinazotolewa na Azam Media Limited kwa sababu wao walikuwa wanapinga kampuni hiyo kupewa Mkataba huo.
  Lakini jitihada zao za kuipinga Azam Media kurusha Ligi Kuu zilishindikana kutokana na ukweli kwamba walitoa ofa nzuri ambayo hakukuwa na kampuni iliyofikia hata nusu yake.
  Yanga SC wakajaribu kutaka kuzuia Azam kurusha mechi zao, hilo nalo likashindikana kwa kuwa ile si Ligi Kuu ya Yanga SC, ni Ligi Kuu ya Tanzania Bara inayomilikiwa na waliosaini Mkataba na Azam Media Limited, TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) na Bodi ya Ligi.
  Tekelezeni sharti, klabu ipate fedha; Mwenyekiti wa Yanga SC, Yussuf Manji kulia akiwa na Makamu wake, Clement Sanga

  Ilikuwa rahisi wao kujiondoa kwenye Ligi wakacheze ligi ambayo haina Mkataba na Azam Media, kuliko kuizuia kampuni hiyo ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake kutekeleza mkataba wao na TFF na bodi ya Ligi.
  Yanga SC wakagomea fedha za mgawo wa haki ya matangazo Sh. Milioni 100 za msimu uliopita, ambazo Azam Media walizikabidhi kwa bodi ya Ligi.
  Na bodi ya Ligi imezipeleka wapi fedha hizo? “Fedha za Yanga SC zipo, tumeziweka katika akaunti maalum, za msimu uliopita na msimu huu, wakizihitaji wakati wowote waziandikie barua ya kuziomba, tuwapatie,”amesema Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Silas Mwakibinga.
  Maana yake- kama Yanga SC wanazihitaji fedha hizo wanaweza kuzipata ndani ya wiki moja- iwapo wataandika barua na fedha zitahamishiwa kwenye akaunti yao, au kupewa hundi moja kwa moja. 
  Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Silas Mwakibinga kulia akiwa na Mtendaji Mkuu wa Azam Media, Rhys Torrington 

  Azam Media Limited waliingia Mkataba wa haki za matangazo ya Televisheni ya Ligi Kuu mwaka jana na TFF kwa pamoja na bodi ya ligi hiyo, wakitoa Sh. Milioni 100 kwa kila klabu, wakati mwaka huu kuna ongezeko la asilimia 10, na kufanya dau la Milioni 110.
  Tayari kwa msimu huu kila timu, kati ya 14 zilizopo kwenye ligi hiyo imekwishaptiwa Sh. Milioni 55, wakati Sh. Milioni 55 nyingine zitatolewa sambamba na mzuguko wa pili wa Ligi Kuu mapema mwakani.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA SC WAPEWA SHARTI MOJA TU WAKITEKELEZA WANALAMBA MILIONI 155 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top