• HABARI MPYA

  Wednesday, September 24, 2014

  KMKM WAENDELEA KUTISHA LIGI YA ZENJI, WAUTAFUNA MTENDE MARA MBILI

  Na Ameir Khalid, ZANZIBAR
  MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya soka Zanzibar KMKM, wamepata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mtende Rangers katika mechi ya Ligi Kuu ya Zanzibar Grand Malt iliyochezwa jioni uwanja wa  Amaan.
  Huo ni ushindi wa pili mfulululizo kwa wanamaji wa KMKM baada ya awali kuitandika Malindi SC idadi kama hiyo ya mabao.
  Mambo yanaonekana kuwa mabaya kwa  Mtende msimu huu, kwani wameshapoteza michezo yao yote miwili, kufuatia awali kufungwa na Mafunzo bao 1-0.


  Mshambuliaji Idi Kambi (aliyekaa) akivua kiatu chake kukibusu baada ya kuifungia KMKM bao la kwanza, huku akipongezwa na wachezaji wenzake.

  KMKM waliuanza mchezo kwa kulisakama lango la wapinzani wao na kufanikiwa kuandika bao la mapema lililofungwa na mchezaji Iddi Kambi katika dakika ya 25, akiunganisha kwa kichwa mpira wa kona.
  Bao hilo liliishtua Mtende Rangers na wakaanza kupanga mashambulizi ya nguvu hadi jitihada zao zikazaa matunda katika dakika ya 30 pale Yahya Said Tumbo aliposawazisha bao hilo kwa njia ya penelti.
  Mwamuzi wa mchezo huo Ramadhani Kibo, alitoa penelti hiyo baada ya mchezaji wa Mtende Ali Rajab kuangushwa kwenye eneo la adhabu.
  Dakika moja kabla ya mapumziko, washika magendo wa KMKM walijihakikishia ushindi kwa bao la pili lililofungwa na Ibrahim Khamis kwa mkwaju wa penelti kufuatia  Yahya Said Tumbo kuunawa mpira ndani ya eneo la adhabu.    
  Kipindi cha pili Mtende walicheza kwa kasi wakihaha kusaka bao la kusawazisha lakini washambuliaji wake wakiongozwa na Yahya Tumbo walishindwa kutumia vyema nafasi nyingi walizozipata.
  KMKM ililiazimika kucheza pungufu baada ya mchezaji wake Khamis Ali kutolewa nje kwa kadi ya pili ya njano.
  Baada ya mchezo huo, walimu wa timu  zote mbili pamoja na mashabiki walimtupia lawama mwamuzi wakidai alichezesha kwa kuzipinda sheria na kanuni za mchezo.
  Ligi hiyo itakuwa mapumziko kesho Alkhamisi na Ijumaa, na kurudi tena keshokutwa kwa mchezo mmoja kwenye uwanja wa Amaan utaozikutanisha timu za Miembeni SC  na Zimamoto. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KMKM WAENDELEA KUTISHA LIGI YA ZENJI, WAUTAFUNA MTENDE MARA MBILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top