• HABARI MPYA

  Friday, September 26, 2014

  SIMBA SC NA YANGA YASOGEZWA WIKI MOJA TU, NGOMA OKTOBA 18 TAIFA

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  MECHI ya watani wa jadi, Simba SC na Yanga SC mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara itapigwa Oktoba 18, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam badala ya Oktoba 12.
  Mechi zote za Oktoba 11 na 12 zimesogezwa mbele kwa wiki moja kupisha mchezo wa kimataifa, kati ya Tanzania na Benin.
  Taifa Stars itashuka uwanjani Oktoba 12 mwaka huu kuikabili Benin katika mechi ya kirafiki ya kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
  Mechi kali daima; Mechi baina ya Simba na Yanga imekuwa na mvuto wa aina yake kwa miaka mingi nchini, pichani ni wachezaji wa zamani wa timu hizo, Abubakar Salum 'Sure Boy' kushoto na Iddi Suleiman 'Meya' kulia katika ya moja za miaka ya 1990 mwanzoni 

  Mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni. Programu ya Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager kwa ajili ya mechi hiyo itatangazwa baadaye na Kocha Mkuu Mart Nooij.
  Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linaendelea na taratibu nyingine kwa ajili ya mechi hiyo ikiwemo usafiri wa Benin kuja nchini, ambapo timu hiyo inatarajiwa kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Oktoba 10 mwaka huu ikiwa na msafara wa watu 28.
  Pambano la Stars na Benin litatanguliwa na mechi ya kudumisha upendo kati ya viongozi wa dini ya Kikristo na Kiislamu.
  Na kwa sababu, TFF imesogeza mbele mechi zilizokuwa zichezwe wikiendi ya Oktoba 11 na 12 na sasa zitachezwa Oktoba 18 na 19.
  Oktoba 18, Polisi Morogoro itamenyana na Mtibwa Sugar Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, Ndanda na Ruvu Shooting Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara, Kagera Sugar na Stand United Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, Coastal Union na Mgambo JKT Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, Mbeya City na Azam FC Uwanja wa Sokoine, Mbeya na Yanga na Simba Taifa.
  Mzunguko huo utahitimishwa na mchezo kati ya Prisons na JKT Ruvu Uwanja wa Sokoine, Mbeya Oktoba 19.
  Zaidi ya hapo, Ratiba ya Ligi Kuu inabaki kama ambayo ilitolewa awali na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC NA YANGA YASOGEZWA WIKI MOJA TU, NGOMA OKTOBA 18 TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top