• HABARI MPYA

  Tuesday, September 23, 2014

  ZIMAMOTO YAENDELEZA DOZI LIGI KUU ZENJI, YAICHAPA 2-1 KIPANGA

  Na Ameir Khalid, ZANZIBAR
  TIMU ya Zimamoto jana imeendelea kutoa dozi kwa timu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Zanzibar Grand Malt baada ya kuichapa Kipanga mabao 2-1 katika uwanja wa Amaan.
  Huo ni ushindi wa pili kwa waokozi hao wa majanga baada ya awali kuizima Chuoni kwa matokeo kama hayo.
  Mchezaji Abdulhamid Ali alianza mapema katika dakika ya tatu kuifungia Zimamoto bao ambalo lilidumu hadi mwisho wa kipindi cha kwanza.
  Kuanza kwa kipindi cha pili, maafande wa Kipanga walianza kutawala mchezo na kulisakama lango la wapinzani wao na kufanikiwa kusawazisha bao hilo katika dakika ya 61 lililofungwa na Adam Abdallah.

  Baada ya hapo, Zimamoto walikuja juu na kulishambulia lango la Kipanga na kuandika bao la ushindi kupitia mchezaji Makame Adam dakika ya 77 baada ya kumramba chenga kipa wa Kipanga Ramadhan Abdalla.
  NAYE ABDI SULEIMAN anaripoti kuwa katika uwanja wa Gombani kisiwani Pemba, timu ya JKU ikawatandika wanajeshi wa Hard Rock mabao 2-0.
  JKU ilifungiwa mabao yake na wachezaji Amour Omar na David Julius dakika ya 19 na 32 mtawalia.
  Ligi hiyo inaendelea tena leo kwa mchezo mmoja kati ya Mafunzo na Malindi  SC utakaopigwa uwanja wa Amaan.
  Kesho pia kutakuwa na mechi moja katika uwanja huohuo, itakayowakutanisha mabaharia wa KMKM na Mtende Rangers.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: ZIMAMOTO YAENDELEZA DOZI LIGI KUU ZENJI, YAICHAPA 2-1 KIPANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top