• HABARI MPYA

  Friday, September 26, 2014

  MALINZI AMPIGA STOP KIPA WA JKT RUVU KUCHEZA LIGI HADI AWASILISHE VIPIMO TFF

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ameizuia klabu ya JKT Ruvu ya Pwani kumtumia kipa Jackson Abraham Chove hadi hapo itakapowasilisha vipimo kwamba hana madhara kichwani baada ya kuumia katika mechi ya ufunguzi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanania Bara mwishoni mwa wiki.
  Chove au Mandanda, alipata dhoruba kichwani katika mechi dhidi ya Mbeya City Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya na kupoteza fahamu kwa zaidi ya dakika ya 10, Jumamosi timu hizo zikitoka 0-0- lakini tayari amekwishaanza mazoezi kwa ajili ya mechi ijayo dhidi ya Kagera Sugar Jumapili, Uwanja wa Azam Complex, Jumapili.
  Akizungumza mchana wa leo wakati wa kukabidhi vyeti kwa wahitimu wa mafunzo ya uongozi kwa viongozi wa vyama vya soka vya wanawake vya mikoa ya Tanzania Bara, Malinzi amesema amefanya hivyo kufuata mwongozo wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
  “FIFA inasema mchezaji akipata pigo la kichwani mchezoni, anatakiwa apimwe na kuthibitishwa hajapata maumivu ya hatari, ndipo aruhusiwe kuendelea kucheza, ili kuepuka kuhatarisha usalama wake,” amesema Malinzi.
  Papa Mandanda; Kipa Jackson Chove amezuiwa kucheza hadi hapo atakapowasilisha vipimo TFF 

  “Sasa nami nimeagiza yule kipa wa JKT Ruvu aliyeumia kichwani kwenye mechi na JKT asiruhusiwe kucheza, hadi klabu yake itakapowasilisha ripoti ya vipimo vyake TFF na kuthibitishwa na TASMA (Chama cha Madaktari wa Michezo Tanzania) kwamba yuko salama ndipo ataruhusiwa kucheza,”aliongeza Malinzi.
  Kwa upande wake, Meneja wa JKT Ruvu, Sajini Taji Constantine Masanja amesema kwamba hawajapata taarifa ya maandishi kutoka TFF, hivyo wanashindwa waanzie wapi kutekeleza hilo.
  “Huyu mchezaji kweli aliumia kwenye mchezo huo, lakini hayakuwa maumivu makubwa amepimwa na kuonekana yuko fiti na tayari ameanza mazoezi kwa ajili ya mchezo ujao,”amesema. 
  Hafla ya kufunga mafunzo hayo imefanyika leo asubuhi kwenye ofisi za TFF, Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
  Mafunzo hayo ya siku tano yalishirikisha viongozi 34 wakiwemo baadhi ya waandishi wa habari na Meneja wa Twiga Stars, na yaliendeshwa na Mkufunzi wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Mtanzania Henry Tandau.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MALINZI AMPIGA STOP KIPA WA JKT RUVU KUCHEZA LIGI HADI AWASILISHE VIPIMO TFF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top