• HABARI MPYA

  Wednesday, September 24, 2014

  PIGO LINGINE SIMBA SC; IVO MAPUNDA AVUNJIKA KIDOLE NA HATADAKA DHIDI YA YANGA OKTOBA 12

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  KIPA namba moja wa Simba SC, Ivo Philip Mapunda amevunjika kidole mazoezini Zanzibar leo asubuhi na anatakiwa kuwa nje kwa wiki nane- maana yake hataweza kusimama langoni timu hiyo ikimenyana na watani, Yanga SC Oktoba 12.
  Daktari wa Simba SC, Yassin Gembe ameiambia BIN ZUBEIRY jioni hii kwamba, Ivo aliumia wakati anachupia mpira katika mazoezi ya asubuhi na kwa bahati mbaya ukamgonga kwenye kidole kidogo cha mwisho mkono wa kulia.
  Majanga; Ivo Mapunda anatakiwa kuwa nje ya Uwanja kwa wiki nane maana yake hatadaka dhidi ya Yanga SC Oktoba 12
  Amesema Ivo alitoka mazoeizini baada ya tukio hilo na baadaye akapelekwa hospitali ya Mnazi Mmoja, ambako baada ya vipimo ikagundulika amevunjika sana.
  “Si kuvunjika kwa mzaha, amevunjika sana na anatakiwa kupumzika kwa wiki nane, baada ya hapo aanze taratibu, ina maana makadirio ya kurudi tena uwanjani ni hadi baada ya miezi mitatu,”amesema Gembe.   
  Kuumia kwa Ivo kunatoa nafasi kwa makipa chipukizi, Hussein Sharrif ‘Cassilas’ na Peter Manyika kujibidiisha ili kuziba pengo lake.
  Ivo anafanya idadi ya wachezaji wanne tegemeo majeruhi Simba SC, baada ya Paul Kiongera anayetakiwa kuwa nje wiki sita, Haroun Chanongo na Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ ambao hawatahitaji zaidi ya wiki ya moja ya kuwa nje ya Uwanja.    Ivo alijiunga na Simba SC Desemba mwaka jana akitokea Gor Mahia ya Kenya na tangu wakati huo amedaka jumla ya mechi 22 za kirafiki na mashindano na kufungwa mabao 15.
  Kabla ya kwenda Kenya, Ivo amewahi kudakia Tukuyu Stars na Prisons zote za Mbeya, Moro United, Yanga SC, St George ya Ethiopia na African Lyon ya Dar es Salaam. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: PIGO LINGINE SIMBA SC; IVO MAPUNDA AVUNJIKA KIDOLE NA HATADAKA DHIDI YA YANGA OKTOBA 12 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top