• HABARI MPYA

  Wednesday, September 24, 2014

  LAZIMA UITAKIE MABAYA SOKA YA TANZANIA KWANZA, KABLA YA KUMTAKIA MABAYA MALINZI

  JUMAPILI niliandika kwamba, haiingii akilini kusema Tanzania ilitolewa na Msumbiji baada ya hujuma- nikielezea kwa muhtasari rekodi baina yetu na wao. 
  Niliweka bayana kwamba, Msumbiji ni nchi ambayo pamoja na kuwa juu yetu kisoka, pia imekuwa na bahati ya kutunyanyasa kwenye mashindano ya kimataifa.
  Nilisema, tangu tuna wachezaji ambao tunaamini ni bora zaidi akina Athumani China, Saidi Mwamba ‘Kizota’ (marehemu), Hussein Marsha na Nteze John Lungu, hatukuweza kufurukuta mbele ya Mambas.

  Msumbiji ilitufunga nyumbani, wakati Marcio Maximo amefanikiwa kuwaunganisha mashabiki wa Tanzania na kuwa kitu kimoja na kuisapoti timu yao kwa nguzu zote.
  Lakini pia nilisema, sitaki kubeza harakati za TFF chini ya rais wake, Jamal Malinzi, zaidi ya kusema kwangu haiingii akilini kama tumetolewa na Msumbiji kwa sababu ya hujuma.
  Hiyo ilihusu mpango wa TFF kufanyia uchunguzi tuhuma za Stars kuhujumiwa na wadau wa michezo nchini ambao wataitwa kuhojiwa katika jopo litakaloundwa na shirikisho hilo la soka nchini.
  Kuna imani upande wa akina Malinzi kwamba wapo watu ambao hawaitakii mema soka ya Tanzania- tu kwa sababu ya chuki zao binafsi na Rais huyo wa TFF.
  Akina Malinzi wanaamini watu hao wanatamani kusikia kila habari mbaya katika soka yetu kwa sasa. Wanatamani kuona mambo yanakwenda ovyo kabisa katika soka yetu kwa sasa.
  Hawataki kuona chochote kizuri kinatokea katika soka ya nchi hii, Rais wa TFF akiitwa Jamal Malinzi.
  Na inasadikiwa wanafanya hivyo, wakiamini wanamkomoa Malinzi- ila kama kweli watu hao wapo, wanasahu tu kwamba bwana mkubwa huyo anaongoza chombo cha Watanzania.
  Malinzi anaongoza soka ya Tanzania, ambayo ikifanya vizuri watakaofurahia ni wananchi wake na ikifanya vibaya watakaohuzunika ni Watanzania.
  Sasa kama kweli watu hao wapo, sijui wao ni Watanzania wa aina gani. Hii itakuwa aina ya upinzani mbaya sana ambayo inaingia kwenye soka yetu kwa sasa.
  Na unaweza kuona kama watu wa aina hiyo wapo, ndiyo inaleta hisia za kuhujumiwa- lakini sasa tujiulize, watu wa aina hiyo wana mapenzi ya mpira wetu kweli?
  Hapana shaka haya ni makovu ya uchaguzi ambayo sasa yanaelekea kuitafuna soka ya Tanzania. Ikumbukwe Malinzi hakushinda na timu yake yote aliyoitaka, kuna watu ameingia nao madarakani ambao hawakuwa sehemu ya timu yake katika kampeni.
  Maana yake hii inaleta hali ya kutoaminiana hata katika utendaji wa kazi pale TFF, sasa tujiulize kama kwa mtaji huu soka yetu ipo katika mwelekeo upi.
  Lazima umefika wakati Watanzania tubadilike- tuweke mbele maslahi ya taifa letu badala ya ubinafsi unaotufikisha hadi kuiombea mabaya nchi yetu wenyewe. 
  Zamani, wazee wetu walikuwa wanasema ‘anayemuoa, mama ndiye baba’- ili kujiridhisha hata pale walipochaguliwa viongozi wasiowataka basi wawaunge mkono na kuwapa ushirikiano.
  Soka ya Tanzania haiwezi kufika popote iwapo sisi wenyewe kwa wenyewe humu hatutapendana na kushirikiana.
  Ubinafsi ni tatizo kubwa katika nchi yetu, ila katika michezo linataka kuvuka mipaka- tunaona katika klabu zetu inafikia watu kweli wanahujumu klabu zifanye vibaya kwa sababu hawamtaki kiongozi aliye madarakani.
  Sasa kama haya mambo yatahamia kwenye timu ya taifa, ni hatari sana. Ni hatari kwa sababu, nchi yenyewe ina wachezaji wachache wanaoonekana kidogo wanafaa, sasa kama hao nao watalishwa sumu ya kuhujumu taifa lao, nini mustakabali wetu? 
  Nataka niwaambie kitu kimoja Watanzania wenzangu, leo hii huwezi kumtakia mabaya Malinzi bila kwanza kuitakia mabaya soka ya Tanzania- sasa kama wapo wanaomchukia Malinzi kiasi cha kuiombea mabaya soka ya nchi hii, basi hao ni maadui wa mchezo huo nchini. Alamsiki. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: LAZIMA UITAKIE MABAYA SOKA YA TANZANIA KWANZA, KABLA YA KUMTAKIA MABAYA MALINZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top