• HABARI MPYA

  Monday, September 22, 2014

  AYA 15 ZA SAID MDOE: BENDI BORA HAIPATIKANI FACEBOOK

  MATUMIZI ya kurasa za Facebook, Twitter, Instagram na mingine ya aina hiyo, ina tija katika kukuza biashara ya mbali mbali ikiwepo biashara ya muziki lakini ni pale tu itakapotumika kwa ufanisi wa hali ya juu.
  Kwa leo nizungumzie matumizi ya mitandao hiyo ya kijamii kwa bendi zetu za dansi na taarab. Kwa bahati mbaya sana zipo bendi pamoja na wasanii wa dansi na taarab ambao wanaamini kwa kupitia kwa kupitia Facebook, Twitter na Instagram basi watafikia kilele cha mafanikio. Wamesahau kuwa kabla ya Facebook, kitu cha kwanza ni ubora wa kazi zao.

  Ukitazama mfumuko wa matumizi ya mitandao hiyo kwa wasanii wa taarab na dansi pamoja na wadau wao, unafarijika sana, lakini ukianza kupitia maandiko yao, unabakia kusikitika na kujionea namna wanavyoshindwa kutumia fursa hizo za bure.
  Kwasasa hivi mtu wala hajali kutengeneza nyimbo mbaya, ili mradi kuna facebook basi wanaamini wanaweza wakageuza tui la nazi kuwa maziwa. Wanajidanganya sana.
  Facebook na wenzake vimegeuzwa kuwa uwanja wa vita – ni matusi na kusifiana ujinga kwa kwenda mbele. Shabiki wa kawaida anashuhudia upuuzi kwenye maandishi yao badala kushuhudia habari muhimu kuhusu kazi zao (wasanii).
  Sisemi kuwa ni bendi zote, wala sisemi kuwa ni wasanii wote au wadau wote, lakini ukweli ni kwamba baadhi yao wamekuwa ni ‘kichefuchefu’. Ni kama vile wako kwenye ulimwengu wasioujua. Mabishano yaliyojaa ukosefu wa hoja ndio zao.
  Wananikumbusha hadithi moja ya zamani ya vipofu wawili waliomkuta tembo kafa, basi wakasikia watu wanasema tembao kafa – vipofu wale waakaanza kumpapasa. Mmoja akaishia kumshika tembo sikio, mwingine akafanikiwa kumpapasa tembo mwili mzima.
  Basi baada ya hapo ubishi wake ulikuwa balaa! Mmoja akasema kumbe tembo  ni mdogo tu eti ukubwa wake ni sawa na ungo. Yule wa pili akasema hapana, tembo ni mkubwa kama gari. Ikaibuka ligi ya ajabu yule aliyesema tembo ni kama ungo hakukubali kurekebishwa hata watu walipotaka kumrudisha ampapase upya tembo, akakataa akiamini katika kile alichokishika. Hakuhitaji kujiridhisha.
  Na hiyo ndio aina ya mijadala inayotawala facebook kutoka kwa baadhi ya wasanii na wadau wa dansi na taarab. Wako wanaofanana na kipofu aliyemshika tembo sikio na wako wanaolingana na yule aliyempapasa tembo mwili mzima.
  Hivi karibuni, hali ya hewa ilichafuka sana kwa makundi ya Wakali Wao Modern Taradance na Mashauzi Classic Modern Taradance – Wadau wao wakachambana kama wehu hadi kupelekea wamiliki wa bendi hizo kuingizwa kwenye matusi yasiyowahusu. Hali kama hii imewahi pia kutokea baina ya wadau wa Twanga Pepeta na Extra Bongo, iliwahi kutokea pia kwa Mashujaa Band na Twanga Pepeta na wakati fulani  wasanii wa bendi hizo na baadhi ya viongozi wao wakaingia mtegoni na kushiriki mijadala michafu isiyo na tija katika biashara zao.
  Matusi baina ya msanii na msanii mwenzake ndio wala usiseme ni balaa. Zipo sababu nyingi sana zinazochochea ujinga huu lakini sababu kubwa ni mtu kutafuta umaarufu kupitia mgongo wa mwenzake. Kwamba bendi fulani au msanii fulani akianzisha bifu na mtu aliye juu yake kimafanikio basi na yenyewe itapanda chati. Ni sawa na zile timu ndogo za soka zinazoamini kuifunga Simba au Yanga inatosha. 
  Kwa mfumo wa soko la biashara ya muziki lilivyo hapa nchini, bendi nyingi zinategemea kuishi kwa ada ya milangoni (kiingilio) au kukodiwa na promota. Kwa bahati mbaya sana wengi miongoni mwa wadau wanaozishabikia bendi hizi kwenye facebook, si waendaji wa ukumbini, kazi ya kubwa ni kusilikiza kazi kwenye vituo vya radio au kuzi-download nyimbo kwenye internet. Kununua CD kwao ni haramu.
  Badala ya wanamuziki na wadau kujiuliza ni kwanini kazi zao haziuziki, wamegeuka kuwa vituko kwenye mitandao ya kijamii kwa hoja zilizojaa vituko.
  Nitumie fursa hii kuwaambia kuwa bendi bora au msanii bora hapatikani facebook. Ubora unapatikana kwa kutengeneza nyimbo nzuri, mikakati mizuri na miundo mbinu ya kisasa na ndio maana wako wasanii wakubwa huwaoni facebook lakini bado wanapendwa na kazi zao zinapendwa.
  Kwa aina hii ya matumizi mabovu ya mitandao ya kijaamii, nashawishika kukubaliana na msemo wa wazee wetu wa zamani: “Kizuri chajiuza, kibaya chajitembeza”. Tukutane tena Jumatatu ijayo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AYA 15 ZA SAID MDOE: BENDI BORA HAIPATIKANI FACEBOOK Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top