• HABARI MPYA

  Monday, September 09, 2019

  SIMBA SC KUMENYANA NA MTIBWA SUGAR IJUMAA UWANJA WA UHURU MECHI YA LIGI KUU

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MCHEZO wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baina ya mabingwa watetezi, Simba SC na Mtibwa Sugar uliokuwa ufanyike Septemba 18, mwaka huu umerudishwa nyuma na sasa utachezwa Ijumaa wiki hii kuanzia Saa 10:00 jioni Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam.
  Taarifa ya Bodi ya Ligi imesema kwamba mchezo umerudishwa nyuma ili kupisha maandalizi ya timu ya taifa kuelekea mchezo wa kuwania tiketi ya Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) ya mwakani dhidi ya Sudan.
  Taifa Stars watakuwa wenyeji wa Sudan Septemba 20 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam katika mchezo wa Raundi ya Pili ya kuwania tiketi ya CHAN 2020 nchini Ethiopia kabla ya kurudiana Oktoba 18 mjini Kampala, Uganda.
  Na kutoa nafasi zaidi kabla ya mchezo wa kwanza baina ya Tanzania na Sudan, Bodi ya Ligi ndio imeamua kuuridisha nyuma mchezo kati ya Simba na Mtibwa Sugar.
  Tayari kila timu imecheza mechi moja tu ya Ligi Kuu msimu huu, Simba SC ikishinda 3-1 dhidi ya JKT Tanzania nyumbani mjini Dar es Salaam na Mtibwa Sugar wakichapwa 3-1 na Lipuli FC ugenini mjini Iringa.
  Kwa ujumla Ligi Kuu itaendelea Jumamosi Namungo FC wakimenyana na Singida United FC Uwanja wa Majaliwa wilayani Ruangwa mkoani Lindi, JKT Tanzania na Lipuli FC Uwanja wa Isamuhyo, Mbweni, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam na Mbao FC dhidi ya jirani zao Biashara United Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
  Jumapili Ndanda FC watakuwa wenyeji wa Mwadui FC Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara, Tanzania Prisons na Ruvu Shooting Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya na Alliance FC na jirani zao, Kagera Sugar FC Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC KUMENYANA NA MTIBWA SUGAR IJUMAA UWANJA WA UHURU MECHI YA LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top