• HABARI MPYA

    Monday, September 16, 2019

    KATWILA AWATEMA KABWILI, ALLY NG’ANZI NA KELVIN JOHN KIKOSI CHA NGORONGORO HEROES

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KOCHA wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Zubery Katwila amewaengua kwenye kikosi chake wachezaji 16 wakiwemo kipa wa Yanga, Ramadhani Kabwili, kiungo Ally Ng’anzi anayecheza Marekani na mshambuliaji Kelvin John ‘Mbappe’ aliye mbioni kujiunga na KRC Genk ya Ubelgiji.
    Kikosi hicho cha Ngorongoro Heroes kinatarajiwa kushiriki michuano ya vijana chini ya umri wa miaka 20 Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Challenge U20) inayotarajiwa kuanza Septemba 21 hadi Oktoba 5 mjini Kampala, Uganda.
    Katika kikosi alichotaja leo, Katwila ambaye pia ni kocha wa Mtibwa Sugar ya Morogoro amewaengua Kabwili, Ng’anzi anayechezea Madison FC ya Daraja la Kwanza Marekani kwa mkopo kutoka Minnesota United FC ya Ligi Kuu nchini humo, ambayo nayo imemchukua kwa mkopo kutoka Vyskov ya Czech.

    Kelvin John (wa pili kutoka kushoto) ameenguliwa kikosi cha Ngorongoro Heroes 

    Mbali na watatu hao, wengine walioenguliwa kutoka kikosi cha awali cha wachezaji 35 ni James Kahimba wa Coastal Union, Kelvin Kijiri wa KMC, Tariq Seif, Lenny Kissu wote wa Biashara United, Yahya Mbegu wa Simba SC, Herbert Lukindo wa Mbao FC, Mohammed Abdallah, Razack Ramadhani, Abubakar Juma wote wa Mtibwa Sugar, Zanda Said, Samuel Jackson, Omar Banda na Agiri Ngoda wote wa Azam FC.
    Kikosi kamili cha Ngorongoro Heroes kitakachoshiriki michuano ya CECAFA U20 kinaundwa na makipa; Ally Salim (Simba SC), Razack Shekimweki (Mtibwa Sugar) na Abdul Suleiman aliyepandishwa kutoka timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys.
    Mabeki ni; Nickson Kibabage (Difaa Hassan El-Jadidi, Morocco), Oscar Maasai (Azam FC), Andrew Simchiba (Coastal Union), Kibwana Shomari (Mtibwa Sugar), Lusajo Mwaikenda (Azam FC), Dickson Job (Mtibwa Sugar) na Gustapha Simon (Yanga SC).
    Viungo ni Onesmo Mayaya (Mtibwa Sugar), Ally Msengi (KMC), Kelvin Nashon (JKT), Wilbroard Maseke (Azam FC), Gadafi Said (Azam FC) na Novatus Dissmas (Biashara United).
    Washambuliaji ni Frank Kahole (Mtibwa Sugar), Tepso Evance (Azam FC), Israel Mwenda (Alliance FC), Kassim Shaaban (Sahare FC) na Said Luyeye (JKT Tanzania).
    Ngorongoro imepangwa Kundi B pamoja na Kenya, Ethiopia na Zanzibar, wakati Kundi A litakuwa na wenyeji, Uganda, Sudan, Eritrea na Djibouti na Kundi B linazikutanisha timu za Burundi, Sudan Kusini Somali. 
    Ngorongoro Heroes itafungua dimba na Ethiopia Septemba 22, kabla ya kumenyana na Kenya Septemba 24 na kumaliza mechi zake za Kundi B kwa kupambana na ndugu zao, Zanzibar Septemba 26.
    Hatua ya Robo Fainali itafuatia Septemba 29, Nusu Fainali Okatoba 2 na Fainali ya michuano ya CECAFA Challenge U20 mwaka 2019 itapigwa Oktoba 5.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KATWILA AWATEMA KABWILI, ALLY NG’ANZI NA KELVIN JOHN KIKOSI CHA NGORONGORO HEROES Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top