• HABARI MPYA

    Saturday, September 28, 2019

    ZESCO UNITED YAIHAMISHIA YANGA SC KOMBE LA SHIRIKISHO BAADA YA KUICHAPA 2-1 LEO NDOLA

    Na Mwandishi Wetu, NDOLA
    BAO la kujifunga la kiungo Mzanzibari, Abdulaziz Makame dakika za mwishoni limeiondoa Yanga SC kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kufungwa 2-1 na wenyeji, Zesco United jioni ya leo Uwanja wa Levy Mwanawasa mjini Ndola, Zambia.
    Kwa matokeo hayo, Yanga inatolewa kwa jumla ya mabao 3-2, kufuatia sare ya 1-1 baina ya timu hizo kwenye mchezo wa kwanza Septemba 14 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    Zesco United inayofundishwa na kocha wa zamani wa Yanga, Mzambia George Lwandamina inaingia hatua ya makundi inayoshirikisha timu 16, wakati timu ya Tanzania itamenyana na moja ya timu zilizovuka Raundi ya Pili ya Kombe la Shirikisho kuwania kucheza hatua ya makundi ya michuano hiyo mingine ya CAF. 
    Mshambuliaji Mnamibia, Sadney Urikhob ameifungia Yanga leo ikichapowa 2-1 na Zesco mjini Ndola

    Makame, mchezaji aliyeibukia kikosi cha vijana cha mahasimu, Simba B kabla ya kwenda kujiendeleza zaidi kisoka kwao, Zanzibar alijifunga dakika ya 79 alipojaribu kuokoa krosi ya Kalengo kutoka upande wa kushoto.
    Zesco waliuanza vizuri mchezo huo na kupata bao la kuongoza kupitia kwa mshambuliaji wao Mkenya, Jesse Jackson Were aliyefunga kwa kichwa dakika ya 25 akimalizia pasi ya kichwa pia ya Winston Kalengo baada ya mpira wa kurusha wa Simon Silwimba kutoka upande wa kulia.
    Yanga SC wakasawazisha dakika ya 31 kupitia kwa mshambuliaji wake mpya kutoka Namibia, Sadney Khoetage Urikhob kwa shuti la mguu wa kushoto akimalizia mpira uliopanguliwa na kipa Jacob Banda, baada ya shuti la Abdulaziz Makame aliyeunga pasi ya Mghana Lamine Moro kufuatia kona ya Mnyarwanda, Patrick Sibomana kutoka kushoto.
    Baada ya Zesco kupata bao la pili, kocha wa Yanga, Mkongo Mwinyi Zahera aliingiza washambuliaji Mzambia Maybin Kalengo, Juma Balinya na Mrisho Ngassa akiwatoa beki Ali Ahmad Ali na viungo Feisal Salum na Sibomana.
    Mabadiliko hayo yaliongeza kasi ya mashambulizi ya Yanga langoni mwa Zesco United, lakini jioni ya leo bahati ilikuwa kwa vijana wa George ‘Chicken ’Lwandamina waliofanikiwa kusonga mbele.
    Na pia kutolewa kwa kadi nyekundu kwa beki Mghana, Lamine Moro aliyeonyeshwa kadi ya pili ya njano dakika ya 90 kulishusha presha ya mashambulizi ya Yanga katika dakika nne za fidia ya muda uliopotea.
    Kikosi cha Zesco United kilikuwa; Jacob Banda, Mwila Phiri, Clement Mwape, Simon Silwimba, Marcel Kalonda, Anthony Akumu, Thabani Kamusoko, John Chingandu/Kondwani Mtonga dk63, Quadri Kola, Winston Kalengo na Jesse Were/Kasumba Umaru dk81.
    Yanga SC; Metacha Mnata, Ali Ahmed Ali/Maybin Kalengo dk84, Ally Mtoni ‘Sonso’, Lamine Moro, Kelvin Yondan, Abdulaziz Makame, Deus Kaseke, Feisal Salum/Juma Balinya dk82, Sadney Urikhob, Papy Kabamba Tshishimbi na Patrick Sibomana/Mrisho Ngassa dk87.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ZESCO UNITED YAIHAMISHIA YANGA SC KOMBE LA SHIRIKISHO BAADA YA KUICHAPA 2-1 LEO NDOLA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top