• HABARI MPYA

    Wednesday, September 18, 2019

    SAMATTA AWEKA REKODI MPYA, ACHEZA NA KUFUNGA MECHI YAKE YA KWANZA LIGI YA MABINGWA

    Na Mwandishi Wetu, WALS-SIEZENHEIM
    MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta jana ameweka rekodi mbili kwa mpigo, kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza na kufunga kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, japo timu yake KRC Genk ilichapwa 6-2 na wenyeji, Red Bull Salzburg ya Austria Uwanja wa Red Bull Arena mjini Wals-Siezenheim.
    Katika mchezo huo wa Kundi E, Samatta ambaye alikuwa anarejea uwanjani baada ya kukosekana kwenye mchezo wa Ligi ya Ubelgiji Ijumaa kufuatia kuumia akichezea timu yake ya taifa – jana alicheza kwa dakika zote 90 na kufunga bao lake dakika ya 52, wakati bao lingine la Genk lilifungwa na beki Mcolombia Jhon Janer Lucumi Bonilla dakika ya 40.

    Mabao ya Red Bull Salzburg yalifungwa na mshambuliaji Mnorway mzaliwa wa England, Erling Haland dakika ya pili, 34 na 45, Mkorea Hwang Hee-Chan dakika ya 36, nyota wa Hungary, Dominik Szoboszlai dakika ya 45 na ushei na beki mkongwe wa Austria, Andreas Ulmer dakika ya 66.
    Samatta ambaye msimu uliopita alikuwa Mtanzania wa kwanza kucheza michuano ya UEFA Europa League jana amejiwekea rekodi mbili mpya, kucheza Ligi ya Mabingwa, tena kuanza na kumaliza katika mechi ya kwanza na kufunga pia.
    Samatta amempiku Kassim Manara aliyekuwa anashikilia rekodi ya muda mrefu ya kuwa Mtanzania pekee aliyecheza michuano ya klabu barani Ulaya, iliyokuwa ikijulikana kama Kombe la Washindi akiwa na klabu ya SK Austria Klagenfurt ambayo sasa imeunganishwa na Kombe la UEFA na kuwa Europa League.   
    Jana Kwa Samatta mwenye umri wa miaka 26 amecheza mechi ya 163 kwenye mashindano yote tangu amejiunga na KRC Genk Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) akiwa amefunga mabao 68 jumla.
    Katika ligi ya Ubelgiji pekee amecheza mechi 128 na kufunga mabao 52, kwenye Kombe la Ubelgiji amecheza mechi tisa na kufunga mabao mawili, katika Super Cup mechi moja, Europa League mechi 24 katika mabao 14 na Ligi ya Mabingwa mechi moja, bao moja.
    Kikosi cha Red Bull Salzburg kilikuwa: Stankovic, Hwang, Szoboszlai/Okugawa dk63, Ramalho, Junuzovic, Ulmer, Minamino, Bernede, Haland/Daka dk73, Wober na Kristensen/Farkas dk84.
    KRC Genk: Coucke, Mæhle, Dewaest, Lucumí, Uronen, Berge, Hrosovsky, Heynen/Onuachu dk86, Ito/Bongonda dk45, Ndongala/Hagi dk73 na Samatta.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SAMATTA AWEKA REKODI MPYA, ACHEZA NA KUFUNGA MECHI YAKE YA KWANZA LIGI YA MABINGWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top