• HABARI MPYA

    Sunday, February 03, 2019

    YANGA SC YAICHOMOLEA ‘JIONI’ COASTAL PUNGUFU, SARE 1-1 MKWAKWANI

    Na Mwandishi Wetu, TANGA
    WENYEJI, Coastal Union wamelazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Yanga SC ya Dar es Salaam katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.
    Matokeo hayo yanayoiongezea pointi moja kila timu, yanaifanya Yanga ifikishe pointi 54 katika mechi 21 ikiendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi saba zaidi ya Azam FC inayofuatia katika nafasi ya pili kwa pointi zake 47 za mechi 20.
    Coastal Union inayofundishwa na mchezaji wake wa zamani, Juma Ramadhani Mgunda inafikisha pointi 29 katika mechi ya 22 na kupanda hadi nafasi ya nane kutoka ya 10.   
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Nassor Mwinchumu aliyesaidiwa na Abdallah Rashid wa Pwani na Charles Simon wa Dodoma, hadi mapumziko Coastal Union walikuwa wanaongoza kwa bao 1-0.
    Bao hilo lilifungwa na mshambuliaji wa zamani wa Simba SC, Hajji Ugando dakika ya 29 akimalizia krosi maridadi ya mchezaji wa zamani wa Zesco United ya Zambia, Ayoub Lyanga kutoka upande wa kulia.
    Mapema tu msaidizi namba moja wa refa Mwinchumu, Rashid alikataa bao lililofungwa na mshambuliaji Heritier Makambo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) akidai alikuwa aameotea.    
    Mwanzoni tu mwa kipindi cha pili Yanga SC walipata pigo baada ya kiungo wake, Feisal Salum ‘Fei Toto’ kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na mkongwe Haruna Moshi ‘Boban’.
    Kwa kuwa na viungo ‘watu wazima’ watupu uwanjani, Boban, Mrisho Ngassa na Mzimbabwe Thabani Kamusoko haikuwa ajabu kasi ya Yanga ilipungua na Coastal Union wakaanza kutawala mchezo.
    Hata hivyo, kwa kutumia uzoefu, Yanga SC inayofundishwa na kocha Mwinyi Zahera kutoka DRC, iliendelea kupeleka mashambulizi langoni mwa Coastal Union, lakini tatizo likawa katika umaliziaji.  
    Coastal Union wakapata pigo dakika ya 74 baada ya mchezaji wake, Issa Abushehe kutolewa kwa kadi nyekundu kufuatia kumchezea rafu beki wa Gardiel Michael akilipa kisasi baada yaye kuanza kuchezewa na mchezaji huyo wa zamani wa Azam FC. 
    Yanga wakatumia mwanya huo wa Coastal Union kucheza pungufu kupata bao la kusawazisha lililofungwa na kiungo Deus David Kaseke aliyetkea benchi kuchukua nafasi ya Nahodha, Ibrahim Ajibu akimalizia mpira ulioingizwa na Matheo Anthony.
    Yanga SC iliongeza kasi ya mashambulizi kusaka bao la ushindi, lakini ama umakini wao ulikuwa mdogo katika umaliziaji, au safu ya ulinzi ya Coastal Union ilifanikiwa kuzuia vyema majaribio yote.
    Coastal Union wakalalamkika kunyimwa penalti dakika ya 81 baada ya Andrew Simchimba kuanguka wakati anadhibitiwa na wachezaji wa Yanga, refa Mwichumu akidai mchezaji huyo alijiangusha na akamuonya kwa kadi ya njano. 
    Kikosi cha Coastal Union kilikuwa; Hussein Sharrif ‘Casillas’, Miraj Adam, Adeyoum Saleh, Ibrahim Mohammed, Bakari Mwamnyeto, Hassan Hamisi, Hajji Ugando/Deogratius Anthony dk72, Mtende Juma, Andrew Simchimba, Ayoub Lyanga na Issa Abusheshe.
    Yanga SC; Ramadhani Kabwili, Paulo Godfrey, Gardiel Michael/Papy Kabamba Tshishimbi dk77, Kelvin Yondani, Abdallah Hajji ‘Ninja’, Feisal Salum/Haruna Moshi dk49, Mrisho Ngassa, Thabani Kamusoko, Heritier Makambo, Matheo Anthony na Ibrahim Ajibu/Deus Kaseke dk70.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC YAICHOMOLEA ‘JIONI’ COASTAL PUNGUFU, SARE 1-1 MKWAKWANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top