• HABARI MPYA

    Sunday, February 24, 2019

    SIMBA IKIMTUMIA IPASAVYO KAGERE ATAKUWA MFUNGAJI BORA LIGI KUU

    Na Frederick Daudi, DAR ES SALAAM
    Miongoni mwa binadamu hatari kwa sasa kwenye ligi kuu ya Tanzania ni Meddie Kagere. Mnyarwanda huyu amekuwa na mchango mkubwa kwenye mafanikio ya Simba msimu huu.
    Katika mechi  nne za mwisho za Simba kwenye michuano yote, Kagere amefunga magoli 5. Mechi hizo ni dhidi ya Mwadui, Al Ahly, Yanga na Azam.
    Mpaka sasa Kagere ameshafunga magoli 11 na anashika nafasi ya tatu nyuma ya vinara Salim Ayee wa Mwadui mwenye mabo 13 na Harieter Makambo wa Yanga mwenye magoli 12. Lakini je wajua? Kuna mambo makubwa mawili ambayo Simba ikiyafanya, tuzo ya ufungaji bora wa TPL itakuwa ni halali ya Meddie.
    Mosi, kumpa jukumu la kupiga mikwaju ya Penalty. Wachezaji wengi wanaoibuka na kiatu cha ufungaji bora kwenye ligi mbalimbali huwa wanafunga magoli mengine kupitia penalty. Je, umesahau kile kilichomsaidia Harry Kane kwenye kombe la dunia nchini Urusi?
    Messi, Ronaldo, Salah na Aguero ni miongoni tu mwa mafowadi ambao wamewahi kubebwa na magoli ya mikwaju hiyo.
    Meddie Kagere anaweza kuinufaisha zaidi Simba SC iwapo itamtumia vizuri

    Ni kweli John Bocco anapiga penati vizuri. Lakini kuna wakati mpiga penati anatakiwa awe ni yule mwenye magoli mengi hasa akiwa katika nafasi nzuri ya kuibuka mfungaji bora.
    Pili, kuchezeshwa mechi nyingi. Kocha wa Simba, Patrick Aussems amekuwa na mazoea ya kuwabadilisha wachezaji hasa kulingana na aina ya mechi husika. Hili ni jambo jema lakini kuna baadhi ya watu ambao hawapaswi kukosa mechi fulani.
    Mathalani, katika mechi ambayo Simba iliifunga African Lyon bao 3-0 pale jijini Arusha, Kagere angecheza pengine angefunga.
    Pamoja na mchango wa akina John Bocco, Emmanuel Okwi na Clotus Chama kwenye kupiga pasi za mwisho na kufumania nyavu, bado Kagere anaendelea kubaki mchezaji tegemeo zaidi katika idara ya uchekaji na nyavu.
    Kagere anaweza akatumia kwa usahihi nafasi nyingi zaidi kadri anavyozipata ukilinganisha na Bocco ambaye kuna aina fulani ya magoli anashindwa kufunga.
    Mshambuliaji huyu wa zamani wa Gor Mahia amekamilika kila idara, sekta na ofisi. Anafungia kichwa, anafungia mguu wa kushoto na kulia pia. Kama hujui, kamuulize Eric Bailly wa Manchester united. Atakusimulia vizuri alichofanyiwa na Kagere.
    Suala la Kagere kuwa mfungaji bora kwenye ligi kuu Tanzania liko mikononi mwa Simba. Yuko tayari kukupa raha wakati wowote. 
    Ukimpa pasi tu, unapata ujumbe usemao: "Imethibitishwa. Umepokea goli murua kutoka kwa Meddie Kagere"  Baada ya hapo, unamwona Kagere amefumba jicho moja na kutetema uwanjani kwa shangwe na bashasha.
    Simba wakimtumia vizuri mshambuliaji huyu, mwishoni mwa msimu huu hutashangaa kusikia kile kipande cha video ya Haji Manara akimtaja Kagere siku ile ya Simba day. "Meddie Kagere......, Meddie Kagere........ Meddie Kagere......"
    (Frederick Daudi ni mwanafunzi wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam kwenye Shule ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC). Anapatikana kwa namba 0742164329 na e-mail defederico131@gmail.com).
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA IKIMTUMIA IPASAVYO KAGERE ATAKUWA MFUNGAJI BORA LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top