• HABARI MPYA

  Sunday, February 03, 2019

  TP MAZEMBE YAWEKA REKODI YA USHINDI LIGI YA MABINGWA

  TIMU ya TP Mazembe jana ilipata ushindi wa rekodi katika historia ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuichapa mabao 8-0 Club Africain ya Tunisia katika mchezo wa Kundi C uliofanyika Uwanja wa Mazembe mjini Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
  Ushindi huo ulitokana na mabao ya Kevin Mondeko Zatu dakika ya 11 na 39, Mika Miche dakika ya 23, Jackson Muleka dakika ya 37 na 61, Tresor Mputu Mabi dakika ya 76 na 83 na Meschak Elia dakika ya 80.
  Na kwa ushindi huo, TP Mazembe inayofundishwa na kiungo wake wa zamani, Pamphile Mihayo Kazembe inaokota pointi tatu za kwanza kwa kishindo, sasa ikiwa nyuma ya CS Constantine ya Algeria yenye pointi sita ionayoongoza kundi hilo, wakati Club Africain inashika mkia ikiwa haina pointi.

  Ikumbukwe Kundi C limebaki na timu tatu tu – na hizo Mazembe, Club Africain na CS Constantine baada ya kuondolewa kwa Ismailia ya Misri kufuatia vurugu za mashabiki wake. 
  Mambo hayakuwa mazuri jana kwa ndugu zao, AS Vita waliolazimishwa sare ya 2-2 na JS Saoura katika mchezo wa Kundi D Uwanja wa Martyrs de la Penteccte mjini Kinshasa.
  AS Vita watajilaumu wenyewe, kwani waliuanza vizuri mchezo huo na kuongoza 2-0 hadi dakika ya 37 kwa mabao ya Kazadi Kasengu dakika ya 14 na Jean-Marc Makusu Mundele, wote wakimalizia pasi za Tuisila Kisinda, lakini wakajiruhusu kusawazishiwa. 
  Mohamed El Amine Hammia alianza kufunga kwa penalti dakika ya 45 kabla ya Sid Ali Yahia Chérif kusawazidha dakika ya 88.
  Sasa Al Ahly inaendelea kuongoza Kundi D kwa pointi zake saba, ikifuatiwa na AS Vita pointi nne, Simba SC pointi tatu na JS Saoura pointi mbili.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TP MAZEMBE YAWEKA REKODI YA USHINDI LIGI YA MABINGWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top