• HABARI MPYA

    Saturday, February 23, 2019

    MTIBWA SUGAR YAVULIWA UBINGWA ASFC, YAPIGWA KWA PENALTI 4-3 NA KMC CHAMAZI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    TIMU ya Mtibwa Sugar imevuliwa ubingwa wa michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) baada ya kufungwa kwa penalti 4-3 kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 90 na KMC katika mchezo wa hatua ya 16 Bora uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi mjini Dar es Salaam.
    Refa wa kike, Jeonesiya Rukyaa alisukumana kwa kifua na kipa wa Mtibwa Sugar, Benedictor Tinocco baada ya mchezaji huyo kukasirishwa na uamuzi wa kurudiwa kwa penalti aliyoiokoa iliyopigwa na mlinda mlango mwenzake, Mrundi Jonathan Nahimana ambaye aliporudia alipofunga.  
    Wengine waliofunga penalti za KMC ni Yussuf Ndikumana, Emmanuel Mvuyekure wote Warundi na Salum Chukwu, wakati Ismail Gambo yake ilipanguliwa na Tinocco.
    Waliofunga penalti za Mtibwa Sugar, timu kutoka Manungu, Turiani mkoani Morogoro ni Salum Kihimbwa, Henry Joseph na Hassan Isihaka, wakati za Nassor Kapama na Shaaban Nditi zilipanguliwa na kipa Mrundi wa timu ya Manispaa ya Kinondoni.  
    Mtibwa Sugar inaingia kwenye orodha ya mabingwa wengine wa michuano hiyo walioshindwa kufika fainali, ambao ni Yanga mwaka juzi na Simba SC mwaka jana.
    Mechi nyingine za hatua ya 16 Bora ya michuano hiyo leo, Kagera Sugar imeifunga 2-1 Boma FC ya Mbeya Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba na Lipuli FC imeichapa 3-1 Dodoma FC Uwanja wa Samora mjini Iringa.
    Mchezo mwingine unafuatia usiku huu Uwanja wa Azam Complex, Chamazi mjini Dar es Salaam kati ya Singida United na Coatsal Union ya Tanga. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MTIBWA SUGAR YAVULIWA UBINGWA ASFC, YAPIGWA KWA PENALTI 4-3 NA KMC CHAMAZI Rating: 5 Reviewed By: Mwakasege Blog
    Scroll to Top