• HABARI MPYA

    Wednesday, February 20, 2019

    YANGA SC YAVUNJA MWIKO KIRUMBA, YATOKA NYUMA NA KUICHAPA MBAO FC 2-1

    Na Mwandishi Wetu, MWANZA
    YANGA SC imetoka nyuma na kushinda 2-1 dhidi ya Mbao FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
    Huo ni ushindi wa kwanza kabisa kwa Yanga dhidi ya Mabo FC Uwanja wa CCM Kirumba, baada ya awali kufungwa mechi zote mbili za msimu uliopita.
    Kwa ujumla katika Ligi Kuu, timu hizo zimekutana mara tano na Yanga imeshinda mechi nne ikiwemo ya leo na zote tatu za Dar es Salaam, wakati Mbao wameshinda mechi mbili zilizopita za Mwanza. 
    Ushindi wa leo unazidi kuwafanya Yanga SC waendelee kuongoza Ligi Kuu, sasa wakifikisha pointi 61 baada ya kucheza mechi 25, wakifuatiwa na Azak FC yenye pointi 50 za mechi 24 na mabingwa watetezi, Simba SC ni wa tatu kwa pointi zao 42 za mechi 17.

    Katika mchezo huo uliokuwa mkali na wa kusisimua, Robert Ndaki alianza kuifungia Mbao FC kwa kichwa dakika ya 45 na ushei akimalizia krosi ya Amos Charles kutoka upande wa kushoto.
    Mshambuliaji Heritier Ebenezer Makambo akaisawazishia Yanga dakika ya 50 kwa kichwa akimalizia krosi ya kiungo Papy Kabamba Tshishimbi, wote wa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
    Na mshambuliaji Mrundi, Amissi Tambwe akaifungia Yanga bao la ushindi kwa penalti dakika ya 68 baada ya beki Erick Muliro wa Mbao FC kuunawa mpira uliopigwa na Kelvin Yondan kwenye boksi.
    Baada ya mabao hayom timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu, ingawa Yanga SC walicheza kwa tahadhari zaidi kuulinda ushindi wao.
    Kikosi cha Mbao FC kilikuwa; Metacha Mnata, Vincent Philipo, Amos Charles, David Mwasa, Erick Mulilo, Ally Mussa, Said Junior, Ibrahim Hashim, Pastory Athanas, Bernard Gervas/Babilas Chitembe na Ndaki Robert/Egbert Lukindo.
    Yanga SC; Ramadhani Kabwili, Paulo Godfrey, Mwinyi Mngwali, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Kelvin Yondan, Papy Kabamba Tshishimbi, Mrisho Ngassa/Mohammed Issa ‘Banka’, Haruna Moshi ‘Boban’, Heritier Makambo, Amissi Tambwe/Andrew Vincent ‘Dante’ na Ibrahim Ajibu/Deus Kaseke.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC YAVUNJA MWIKO KIRUMBA, YATOKA NYUMA NA KUICHAPA MBAO FC 2-1 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top