• HABARI MPYA

    Wednesday, February 20, 2019

    MAKONDA KUONGOZA KAMATI YA KUISAIDIA TAIFA STARS IFUZU AFCON 2019

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) leo imetaja Kamati maalum ya watu 14 kwa ajili ya kuisaidia timu ya taifa, Taifa Stars ifuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika kuanzia Juni 21 hadi Julai 19 mwaka huu nchini Misri.
    Taarifa ya TFF leo imesema kwamba, Kamati hiyo itaongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda atakayekuwa Mwenyekiti, huku Katibu wake akiwa Mhandisi Hersi Said.
    Wajumbe wa Kamati hiyo ni wafanyabiashara Mohamed ‘Mo’ Dewji, Farouk Baghodha, Salum Abdallah ‘Try Again’, Mohammed Nassor, Patrick Kahemele, Abdallah Bin Kleb, Teddy Mapunda, Philemon Ntahilaja, Farid Nahid na Faraji Asas.
    Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ataongoza Kamati ya kuisaidia Taifa Stars ifuzu AFCON

    Jukumu kubwa ya kamati hiyo itakuwa ni kuhakikisha Taifa Stars inapata ushindi katika mchezo wa mwisho wa Kundi L kuwania tiketi ya AFCON dhidi ya Uganda Machi 22 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    Siku hiyo kutakuwa na mchezo mwingine wa Kundi L kati ya Cape Verde na Lesotho, timu nyingine katika mbili katika kundi hilo.
    Uganda ndiyo inaongoza kundi hilo na tayari imejihakikishia tiketi ya Misri katikati ya mwaka huu kwa pointi zake 13, ikifuatiwa na Lesotho yenye pointi tano sawa na Tanzania, wakati Cape Verde ina poinyi nne baada ya timu zote kucheza mechi tano.
    Taifa Stars itafuzu moja kwa moja iwapo itashinda dhidi ya Uganda na Cape Verde itaifunga Lesothi au kutoa sare.
    Kama Lesotho itaifunga Cape Verde hata Taifa Stars ikiifunga Uganda haitakwenda Misri kwa sababu ya sharia ya kutazama matokeo ya mechi zilizokutanisha timu zilizofungana kwa pointi, kwani Tanzania ilifungwa ugenini na kutoa sare nyumbani. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MAKONDA KUONGOZA KAMATI YA KUISAIDIA TAIFA STARS IFUZU AFCON 2019 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top