• HABARI MPYA

    Wednesday, February 13, 2019

    AZAM FC YAPANIA KUIPIGA TANZANIA PRISONS KESHO UWANJA WA SOKOINE

    Na Mwandishi Wetu, MBEYA
    KIKOSI cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, tayari kimewasili salama mkoani Mbeya kikiwa kimejidhatiti kufanya kweli kwenye mchezo ujao dhidi ya Tanzania Prisons.
    Azam FC inawasili mkoani humo ikiwa imetoka kucheza mkoani Iringa dhidi ya Lipuli jana Jumatatu, ikipata sare ya bao 1-1 huku bao lake likifungwa na kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’.
    Akizungumza leo mjini hapa, Kocha Msaidizi wa Azam FC, Juma Mwambusi, aliwapongeza wachezaji kwa kutoka nyuma na hatimaye kupata sare ya ugenini.
    Juma Mwambusi, aliwapongeza wachezaji kwa kutoka nyuma na hatimaye kupata sare ya ugenini na Lipuli
    Kocha Mkuu, Mholanzi Hans van der Pluijm akiongoza mazoezi leo

    Mshambuliaji Mzimbabwe, Donald Ngoma akiwa mazoezini leo

    “Mchezo ulikuwa ni mzuri na mgumu, Azam kipindi cha kwanza hatukuweza kucheza vizuri kwa sababu wachezaji waliingia kwenye mchezo wakiwa na kasi ya chini, kwa kiasi kikubwa ilichangiwa na hali ya uwanja kwa sababu ilinyesha mvua kabla ya mpira kuanza kwa hiyo walicheza kwa tahadhari zaidi ili wasiweze kupata majeraha na kusababisha matatizo langoni,” alisema.
    Alisema waliweza kufanya mabadiliko kipindi cha pili kwa kucheza mpira wa kushambulia kutokea pembeni na katikati hadi kufanikiwa kusawazisha bao wailotanguliwa kipindi cha kwanza na Lipuli.
    “Pengine tungeweza kutulia zaidi kwa washambuliaji wetu tungeweza kushinda mabao mawili au matatu na kuondoka na pointi tatu katika mechi hii, yote kwa yote tunajipanga kwa mchezo unaokuja (Tanzania Prisons,” alisema.
    Mara baada ya kikosi cha Azam FC kuwasili mkoani Mbeya, kesho Jumatano kinatarajia kufanya mazoezi ya mwisho kwenye Uwanja wa Sokoine kabla ya kuvaana na maafande hao.
    Matokeo ya jana yameifanya Azam FC kufikisha jumla ya pointi 49 ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikizidiwa pointi tisa na vinara Yanga waliokuwa nazo 58, lakini matajiri hao wakiwa na mchezo mmoja mkononi.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM FC YAPANIA KUIPIGA TANZANIA PRISONS KESHO UWANJA WA SOKOINE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top