• HABARI MPYA

    Tuesday, February 26, 2019

    FIFA YAMFUNGIA MAISHA REFA WA TANZANIA KWA RUSHWA NA UPANGAJI MATOKEO

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KAMATI ya Maadili ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) chini ya Mwenyekiti wake, Vassilios Skouris imemfungia maisha Mwamuzi wa zamani wa Kimataifa na Katibu wa Chama Cha Waamuzi Tanzania (FRAT), Oden Charles Mbaga baada ya kutiwa hatiani kwa rushwa na upangaji matokeo.
    Afisa Habari na Mawasiliano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Cliford Mario Ndimbo amesema leo mjini Dar es Salaam kwamba baada ya uchunguzi uliofanyika kuanzia Julai 11, 2018 Mbaga amekutwa na hatia ya kuhusika kwenye upangaji wa matokeo ikiwa ni kinyume na kanuni za Maadili za FIFA.
    Mbaga amevunja Ibara ya 11 ya Kanuni ya rushwa ya FIFA ya mwaka 2009. Anafungiwa maisha kutojihusisha na shughuli zozote za Mpira wa Miguu katika ngazi ya Kitaifa na Kimataifa kwa mujibu wa Ibara ya 7j ya Kanuni za Maadili za FIFA za mwaka 2018 pamoja na Ibara ya 22 ya Kanuni ya Nidhamu ya FIFA.

    Refa Oden Charles Mbaga (katikati) amefungiwa maisha baada ya kutiwa hatiani kwa rushwa na upangaji matokeo

    Aidha Mbaga anatakiwa kulipa faini ya kiasi cha fedha ya Uswis Faranga 200,000 ndani ya siku 30 tokea amepata taarifa hizo na anaweza kulipa kwa fedha ya Swiss au kwa dola za Kimarekani.
    Vilevile Mbaga anatakiwa kulipa gharama za shauri hilo kiasi cha Faranga za KiSwiss 1,000 ndani ya siku 30 tokea amepata taarifa.
    Anaweza kukata rufaa kwenye mahakama ya kimichezo ya FIFA CAS,rufaa ambayo inawasilishwa moja kwa moja CAS ndani ya siku 21 tokea maamuzi yalipofanyika na ndani ya siku 10 baada ya kumalizika siku 21.
    Mbaga ambaye ni Katibu wa Chama cha Waamuzi Tanzania (FRAT) anapoteza sifa ya nafasi hiyo kutokana na adhabu ya kufungiwa maisha kutojihusisha na masuala ya Mpira wa Miguu.


    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: FIFA YAMFUNGIA MAISHA REFA WA TANZANIA KWA RUSHWA NA UPANGAJI MATOKEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top