• HABARI MPYA

    Sunday, February 17, 2019

    UTABIRI WA ZAHERA UMETIMIA, YANGA INAANGUSHWA NA VIONGOZI

    MSHAMBULIAJI Mnyarwanda mwenye asili ya Uganda, Mohammed ‘Meddie’ Kagere jana aliibuka shujaa baada ya kuifungia Simba SC bao pekee ikiwalaza mahasimu wao wa jadi, Yanga 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    Ushindi huo unawafanya Simba SC wafikishe pointi 39 baada ya kucheza mechi 16, ikipanda hadi nafasi ya tatu kutoka ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu, sasa ikizidiwa pointi 10 na Azam FC na 19 na Yanga SC wanaoongoza, baada ya wote kucheza mechi 23.  
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Hance Mabena aliyesaidiwa na washika vibendera Mohammed Mkono, wote wa Tanga na Kassim Mpanga wa Dar es Salaam, Kagere alifunga bao hilo dakika ya 72 kwa kichwa akiruka katikati ya mabeki wa Yanga Abdallah Shaibu ‘Ninja’ na Paulo Godfrey ‘Boxer’ kuunganisha krosi ya Nahodha John Raphael Bocco.
    Pamoja na kuanza na washambuliaji watatu, Mrundi Amissi Tambwe, Heritier Makambo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na mzawa, Ibrahim Ajibu, lakini Yanga kwa mara nyingine leo imecheza kwa kujilinda zaidi, ikishambulia kuwa kushitukiza.
    Angalau jana ilitengeneza mashambulizi ya nguvu tofauti na Septemba 30 ikifanikiwa kupata sare ya 0-0 na Simba, lakini mshambuliaji wake Makambo hakuwa na bahati kutokana na kupoteza nafasi mbili za wazi, moja kila kipindi.  
    Dakika ya 39 Makambo aliye katika msimu wake wa kwanza Yanga SC, aliunganishia nje kwa kichwa krosi nzuri ya Ibrahim Ajibu kutoka upande wa kulia ambayo iliwapita mabeki wa Simba na kipa wao, Aishi Manula.
    Na Amissi Tambwe akaonyeshwa kadi ya njano dakika ya 45 kwa kujaribu kuucheza mpira kwa mkopo akiwa kwenye boksi la Simba. 
    Dakika ya 87 Makambo tena akapatwa na kigugumizi cha miguu akiwa amebaki na kipa Aishi Manula baada ya kupenyezewa pasi nzuri na Mrisho Ngassa hadi kipa huyo akapangua kabla ya beki Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ kuondoa kwenye hatari.
    Lakini ni Simba SC iliyotawala zaidi mchezo kwa ujumla jana, hususan baada ya mabadiliko ya mapema kipindi cha pili, Hassan Dilunga ‘HD’ akiingizwa kwenda kuchukua nafasi ya kiungo Mzambia, Clatous Chama.
    Dakika ya 58 Okwi alipiga shuti kali likagonga mwamba wa juu na kwenda nje, kabla ya Jonas Mkude naye kufumua shuti dakika moja baadaye likaenda mikononi mwa kipa chipukizi wa Yanga, Ramadhani Awam Kabwili.
    Shambulizi kali zaidi la Simba langoni mwa Yanga lilikuwa dakika ya 65 wakati Bocco alipounganisha kwa kichwa krosi ya Tshabalala, lakini Abdallah Shaibu ‘Ninja’ akaokoa, Kagere akajibu kwa shuti na beki huyo akaokoa tena katika mstari.
    Kwa ujumla Simba ilipiga mashuti matatu yaliyolenga lango dhidi ya moja la Yanga, 11 yaliyokwenda nje dhidi ya matano huku ikipiga kona nne dhidi ya mbili wapinzani wao.
    Mwishoni mwa mchezo mchezo kiungo wa Yanga, Feisal Salum ‘Fei Toto’ alimsukuma Kagere wakati anatoka taratibu baada ya kufanyiwa mabadiliko kumpisha Mnyarwanda mwenzake, Haruna Niyonzima.
    Refa alimuonya kwa kadi ya njano Kagere kwa kujichelewesha kutoka na akawa mchezaji wa tatu wa Simba kuonyeshwa kadi hiyo baada ya beki Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Emmanuel Okwi.
    Mabena pia aliwaonyesha kadi za njano wachezaji wanne wa Yanga, Gardiel Michael, Kelvin Yondan, Feisal Salum na Tambwe.  
    Kipigo hicho kinakamilisha utabiri wa kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) alioutoa mapema Desemba mwaka jana baada ya dirisha dogo la usajili kufungwa, huku uongozi ukishindwa kusajili wachezaji aliowahitaji.
    Zahera alitaka kusajiliwa, kipa, kiungo na mshambuliaji, wote wa kigeni – lakini badala yake uongozi ukamsajili mchezaji mkongwe Haruna Moshi ‘Boban’ na aliyekuwa anacheza soka ya ufukweni, Ibrahim Hamid. 
    Akasikitishwa zaidi na kitendo cha uongozi kushindwa hata kumsajili winga wa Stand United, Charles Ilamfya aliyesajiliwa na KMC ya Kinondoni. Na kwa sababu hiyo, Zahera akasema akifungwa na Simba asiulizwe na hata akiukosa ubingwa asiulizwe pia.
    Tayari Yanga SC imefungwa na Simba SC ikitoka kushinda mechi moja tu ya nne zilizopita – na baada ya utabiri wa kwanza wa Zahera kutimia tutaraije hata ndoto za ubingwa Yanga ndiyo zimeyeyuka kutokana na makosa ya uongozi wakati wa usajili.
    Wapenzi na wanachama wa Yanga wanaipenda timu yao na wanajitahidi kuichangia kwa hali na mali, lakini siku zote wanaangushwa na unaoitwa uongozi.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: UTABIRI WA ZAHERA UMETIMIA, YANGA INAANGUSHWA NA VIONGOZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top