• HABARI MPYA

    Saturday, July 15, 2017

    YANGA SC YAZIDI KUIMARISHA IDARA ZAKE NYETI

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    SIKU moja baada ya kumtangaza Dissmas Ten, kuwa Mkuu mpya wa Idara yake ya Habari na Mawasiliano, klabu ya Yanga imemuongezea mkataba Mkurugenzi wake wa Fedha, Baraka Deusdedit baada ya kazi nzuri iliyothibitika.
    Baraka, kijana mdogo tu wa umri wa miaka 31, amesaini mkataba wa miaka miwili leo, kuendelea kuitumikia Idara ya Fedha ya Yanga kama kiongozi Mkuu, huku akiishukuru klabu kwa uaminifu wake kwake.
    Katika taarifa yake fupi kwa vyombo vya Habari leo, Baraka amesema kwamba anamshukuru Mungu kwa kuongeza mkataba wa kuitumikia Yanga, klabu yake kipenzi tangu utotoni. Amesema hiyo ni changamoto nyingine kwake, kuendelea kufanya kazi nzuri kwa maslahi ya klabu.
    Baraka Deusdedit aliajiriwa Yanga SC Desemba mwaka 2014 kama Mkurugenzi wa Fedha kwa pamoja na Katibu Mkuu, Dk. Jonas Tiboroha.
    Baraka Deusdedit leo amesaini mkataba mpya kuendelea kuwa Mkurugenzi wa Fedha wa Yanga
    Brazameni mchapa kazi; Pamoja na umri wake wa miaka 31 tu, lakini Baraka Deusdedit ni hodari wa kazi

    Hata hivyo, Tiboroha akaondolewa Januari mwaka jana na Baraka Deusdedit akakaimu nafasi ya Ukatibu Mkuu Yanga SC hadi Januari mwaka huu alipompisha Charles Boniface Mkwasa, yeye akirejea kuongoza Idara yake ya Fedha.  
    Baraka amejijengema heshima kubwa Yanga kutokana na mapenzi yake ya dhati aliyoonyesha kwa klabu, uwajibikaji mzuri na uvumilivu pia.
    Katika kipindi kigumu kabisa baada ya aliyekuwa Mwenyekiti, Yussuf Manji kuingia matatizoni na Serikali na baadaye kujiondoa kwenye klabu hiyo, Baraka alishikamana na Katibu Mkwasa, kuhakikisha wanatafuta fedha ili kuweza kuendesha klabu.
    Katika jitihada zao zilizowafanya wabishe hodi sehemu mbalimbali kuomba ufadhili, ndipo wakafanikiwa kuipata kampuni ya SportPesa, wadhamini wapya wa klabu kwa sasa kwa dau la Sh. Bilioni 1 kwa mwaka, kwa miaka mitano.
    Bin Zubeiry Sports – Online inafahamu pia kwamba kwa juhudi za Baraka na Mkwasa, Yanga ipo katika hatua za mwishoni kukamilisha dili mbili za udhamini na kampuni nyingine tofauti nchini. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC YAZIDI KUIMARISHA IDARA ZAKE NYETI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top