• HABARI MPYA

    Sunday, July 30, 2017

    'CHAMPION BOY' SAMATTA KAMA KAWAIDA, AANZA MSIMU MPYA NA BAO

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta ‘Champion Boy’ ameuanza msimu mpya wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji kwa kufunga katika sare ya 3-3 na Waasland-Beveren Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk.
    Waasland-Beveren waliuanza mchezo kwa kasi na kufanikiwa kuongoza kwa mabao 2-0 hadi baada ya mapumziko wafungaji Olivier Myny dakika ya 45 na Zinho Gano dakika ya 47.
    Lakini Genk wakazinduka na kukomboa mabao hayo kupitia kwa Jose Naranjo dakika ya 70 na  Samatta dakika ya 80 kabla ya Mtanzania huyo kumsetia Siebe Schrijvers kufunga bao la tatu dakika ya 82.
    Mbwana Samatta (kushoto) akikimbia na wenzake baada ya kuisawazishia Genk na kuwa 2-2 kabla ya mchezo kumalizika kwa sare ya 3-3
    Mbwana Samatta (juu kulia) akipambana katika mchezo huo uliokuwa mkali 

    Hata hivyo, wakati Genk wakiamini wataondoka na pointi tatu, wakajikuta wanachomolewa bao dakika ya mwisho ya mchezo, baada ya Zinho Gano tena kuifungia Waasland-Beveren dakika ya 90 na ushei.
    Mchezo wa leo umekuwa wa 56 kwa Samatta katika mashindano tangu Januari mwaka jana alipojiunga na Genk akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC, kati ya hiyo 34 akianza na 21 akitokea benchi.
    Katika mechi hizo, mshambuliaji huyo wa zamani wa African Lyon, zamani Mbagala Market na Simba zote za Dar e Salaam, amefunga jumla ya mabao 19 huku akionyeshwa kadi za njano mara nne na hajawahi kutolewa kwa kadi nyekundu.
    Kikosi cha KRC Genk kilikuwa: Jackers, Brabec, Nastic, Khammas/Maehle dk62, Colley, Berge, Malinovskyi/Naranjo dk66, Trossard, Benson/Writers dk45, Buffalo na Samatta
    W.-Beveren: Goblet, Demir, Moren, Gano, Seck, Jans, Ampomah/Cerigioni dk75, Cools, Myny/Boljevic dk63, Morioka na Camacho.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: 'CHAMPION BOY' SAMATTA KAMA KAWAIDA, AANZA MSIMU MPYA NA BAO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top